Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemkuta na kesi ya kujibu Sophia Mwenda (64) na mwanaye wa kiume Alophonce Magombola (39), hivyo wanatakiwa kujitetea.
Sophia na mwanaye wanadaiwa kumuua Beatrice Magombola, ambaye ni binti yake wa kwanza wa kumzaa mwenyewe kwa kumchoma kisu chini ya titi, tukio wanalodaiwa kulitenda Desemba mosi, 2020 Kijichi, wilaya ya Kigamboni.
Uamuzi huo umetolewa jana Julai 11, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio, aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi ya mauaji, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.
Upande wa mashtaka uliita mashahidi 22 na vielelezo tisa ambao walitoa ushahidi wao mahakamani hapo kuhusiana na kesi hiyo ya mauaji.
“Baada ya kupitia mashahidi na vielelezo vilizotolewa, mahakama hiyo imeona mna kesi ya kujibu washtakiwa wote, hivyo wanapaswa kujitetea dhidi ya tuhuma zinazowakabili,” alisema Hakimu Mrio.
Hata hivyo mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Hilda Mushi na Godwin Fissoo, waliieleza mahakama hiyo wanatarajia kuwa na mashahidi wanne kila mmoja wakiwemo washtakiwa hao pamoja na vielelezo.
Baada ya kutoa maelezo hayo, mshtakiwa kwa kwanza katika kesi hiyo, Alphonce alianza kutoa utetezi wake.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa utetezi Hilda Mushi, Alphonce alidai kuwa hajawahi kupelekwa Bagamoyo kwenda kuonyesha askari Polisi sehemu ambayo mwili wa Beatrice ulitupwa na kama ingekuwa ni kweli basi hata mwenyekiti wa eneo hilo au askari polisi wa Bagamoyo wangekuja kutoa ushahidi wao.
Pia, hajawahi kupelekwa Kijichi kwenda kuchora ramani ya tukio la mauaji kama mashahidi wa upande wa mashtaka walivyodai na
Vilevile amedai kuwa hajawahi kuhojiwa na polisi kuhusiana na mauaji ya Beatrice kama ambavyo mashahidi wa upande wa mashtaka walivyotoa ushahidi wake wala hajawahi kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hizo.
Akiendelea kutoa utetezi wake, Alphonce alidai kuwa yeye anakumbuka alihojiwa polisi kuhusiana na wizi wa vipuri vya gari, kazi ambayo alikuwa anaifanya kwa wakati huo.
Mshtakiwa baada ya kumaliza kujitetea mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Julai 24, itakapoendelea kwa upande wa utetezi kuendelea kujitetea.
Katika maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo na mashahidi wa upande wa mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kumuua Beatrice na kisha mwili wake kwenda kuutupa eneo la Zinga, lililopo Bagamoyo mkoani Pwani, tukio wanalodaiwa kulitenda Disemba 1, 2020 eneo la Kijichi wilaya ya Temeke.
Hata hivyo, Sophia katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa Kituo cha Polisi Oysterbay, alikiri kumuua mtoto wake ili asiende kutoa ushahidi katika kesi iliyofunguliwa na baba yake Beatrice ambayo inatokana na Sophia kuuza nyumba iliyopo Mbeya akishirikiana na Alphonce, bila kushirikisha familia.
Miongoni mwa mashidi hao wa upande wa mashtaka waliotoka ushahidi wao yupo baba mzazi wa marehemu Beatrice, Douglas Magombola ambaye aliieleza mahakama jinsi alivyopata taarifa za kifo cha mtoto wake huyo, huku akitokwa na machozi baada ya kuoneshwa picha enzi za uhai wake.
Magombola ambaye ni Mhadhiri Mstaafu chuo cha Tengeru, amedai alimuoa Sophia mwaka 1986, na walibahatika kupata watoto wanne ambao ni Beatrice, Alphonce, Rechal na Deslius maarufu Mwila na walitalikiana mwaka 2008.
Amedai taarifa za kifo cha mwanaye alizipata mwaka 2022, kutoka kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam na kipindi hicho, Beatrice alikuwa akiishi na Sophia na mtoto wake.
Magombola alidai, Desemba Mosi, 2020 asubuhi, ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana na Beatrice, walizungumza kuhusu kesi aliyoifungua mahakamani kutokana na Sophia kuuza nyumba ya familia iliyopo Mbeya.
Kwamba Beatrice alitakiwa kwenda kutoa ushahidi Desemba 7, 2020.
“Nilimtafuta Desemba 2, sikumpata hewani, niliendelea kumtafuta bila mafanikio, nilizani mama yake (Sophia), amemzuia asije kutoa ushahidi, niliendelea kumtafuta kazini kwake Ofisi za Tasaf wakanambia ameshamaliza mkataba, nilimtuma mtoto wa kaka yangu anaitwa Mariam akamwangalie katika makazi yake Kijichi, akaambiwa ameshahama, nilimpigia Sophia hakuwa hewani,” amedai Magombola.
“Nilikuja Dar es Salaam, Polisi waliniambia Sophia na Alphonce ndio wanatuhumiwa kumuua Beatrice, walinichukua sampuli kwangu kwa ajili ya kipimo cha vinasaba, pia tulienda kufukua mwili wa Beatrice katika makaburi ya Bagamoyo eneo la Ukuni, tulipofika na kuonyeshwa kaburi mimi sikuweza kustahimili, niliishiwa nguvu, nikarudishwa nyumbani kutibiwa,” amedai Magombola.
Shahidi mwingine ni Mchunguzi kutoka Maabara ya Mkemia Kuu ya Serikali, Leonidas Michael (34), ambaye alifanya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kwa kuchukua taya la marehemu Beatrice na sampuli za mpanguso wa kinywa kwa watu watatu ambao ni washtakiwa wawili pamoja na baba wa marehemu.
Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, sampuli hizo zilionyesha kuwa watu hao ni ndugu wa damu.
Amedai Aprili 12, 2022, akiwa kazini kama Ofisa wa zamu, alipokea kifurushi kutoka kwa askari wa Jeshi la Polisi aitwaye Donald Jackson. Kifurushi hicho kilikuwa kimefungwa kwa lakili (utepe maalumu wa kufungia vielele) na kuambatanishwa na barua kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni, ikieleza yaliyomo.
“Nilikikagua kifurushi hicho mbele ya askari huyo na kubaini kuwa kilikuwa na taya moja la binadamu pamoja na sampuli za mipanguso mitatu ya kinywa kutoka kwa Sophia Mwenda, Doglas Magombola na Alphonce Magombola,” amedai Michael.
Ameongeza kuwa, baada ya kujiridhisha kuhusu ubora wa vielelezo hivyo, aliipa kila sampuli namba ya maabara, kisha kuosha taya hilo kuondoa uchafu na kulikausha kwa hatua za uchunguzi zaidi.
“Nililisaga taya hilo pamoja na meno kwa kutumia ‘blender’ maalum ili kupata unga kwa ajili ya kuchanganywa na kemikali ya ‘Antihuman’ lengo ilikuwa ni kubaini kama kweli ni sehemu ya mwili wa binadamu au la. Majibu yalibainisha hilo baada ya rangi ya Zambarau kuonekana,” amedai Michael.
Michael ameendelea kudai kuwa alichambua sampuli hizo kwa hatua ya kuchenjua vinasaba (DNA extraction), kuongeza wingi (amplification) na hatimaye kuzisoma kwenye mashine maalumu ya kisasa.
“Nilipata ‘low data’ lakini yenye ubora wa kutosha kuniwezesha kupata mpangilio wa vinasaba kwa sampuli zote nne. Nilifanya ulinganisho wa takwimu na matokeo yalionyesha kwamba sampuli hizo zina uhusiano wa kindugu,” amedai
Amebainisha kuwa sampuli ya taya (iliyopewa jina la ‘Z’) ilibainika kuwa ya mtu wa jinsia ya kike, na kuwa na uhusiano wa karibu wa damu na sampuli zilizochukuliwa kwa watuhumiwa pamoja na baba wa marehemu
Shahidi huyo alidai kuwa Julai 7, 2022 aliandaa taarifa fupi ya uchunguzi, kuisaini na kuiwasilisha kwa Meneja wake kwa ajili ya kuhakikiwa kabla ya kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Maabara kwa idhini ya mwisho. Baada ya hapo, taarifa hiyo ilirudishwa kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi.