Mwenge kukagua miradi 51 ya Sh71.3 bilioni  Manyara

Simanjiro. Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 utakagua, kuzindua na kutembelea miradi 51 ya maendeleo yenye thamani ya Sh71.3 bilioni katika Mkoa wa Manyara.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amesema hayo kwenye mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro, leo Jumamosi Julai 12, 2025, wakati akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi.

Sendiga amesema ukiwa katika Mkoa wa Manyara, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 1,197.10 kupitia halmashauri saba za Simanjiro, Kiteto, Babati Vijijini, Babati Mjini, Mbulu Mjini, Mbulu Vijijini na Hanang’.

Amesema Mwenge wa Uhuru unatarajia kuweka mawe ya msingi katika miradi 11 ya thamani ya Sh9.7 bilioni, kuzindua miradi 16 ya thamani ya Sh5.5 bilioni, na kufungua mradi mmoja wa thamani ya Sh98.4 milioni.

Amesema Mwenge wa Uhuru utakagua na kuona miradi 23 ya thamani ya Sh55.9 bilioni, ikiwa ni pamoja na nguvu za wananchi Sh330 milioni.

Ameeleza kwamba, kati ya fedha hizo Sh71.3 bilioni, Serikali Kuu imetoa Sh62.2 bilioni, na mamlaka za Serikali za mitaa kupitia mapato ya ndani zimetoa Sh1.9 bilioni, huku wadau wengine wakichangia Sh6.9 bilioni.

“Nawashukuru na kuwapongeza watu wa Mkoa wa Manyara kwa kuibua, kuanzisha, kuchangia na kuitekeleza miradi hiyo ya maendeleo,” amesema Sendiga.

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2025, Ismail Ussi, amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani.”

“Mwaka huu wa 2025, tujitokeze kwa wingi kupiga kura za mgombea wa urais, wabunge na madiwani ili tupate maendeleo zaidi kupitia hao,” amesema Ussi

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Happy Kayumbo, amesema watu wa eneo hilo wameupokea vyema Mwenge wa Uhuru katika mbio zake kwa mwaka 2025.

“Pia mji umechangamka, kwani mama lishe na baba lishe wameuza vyakula, vituo vya mafuta vimeuza, nyumba za kulala wageni zimepokea wageni na vijana wa bodaboda wamepata fedha pia,” amesema.

Related Posts