Hai. Mchezaji wa zamani wa Major League Baseball (MLB) nchini Marekani, Ryan Kalish, amesema utajiri wa kweli kwa binadamu haupimwi kwa umaarufu au mali alizonazo, bali kwa namna anavyogusa maisha ya wengine.
Kalish, aliyewahi kuichezea timu ya Chicago Cubs kati ya mwaka 2014 na 2016, amesema hayo alipotembelea Taasisi ya New Life Foundation, iliyopo wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, Juni 11, 2025, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuona mazingira halisi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
“Kujikusanyia umaarufu na mali kunaleta furaha ya muda kwa mtu binafsi, lakini kugusa maisha ya wengine na kuwasaidia kubadili hali zao, huo ndiyo utajiri wa kweli,” amesema Kalish huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano na upendo ndani ya jamii.
Amesema tangu astaafu michezo miaka saba iliyopita, amejikita kwenye huduma za kijamii na uinjilishaji, akilenga kuwahamasisha watu kuonyesha upendo bila kujali mipaka ya kijamii wala kitaifa.
“Dunia inahitaji upendo. Tunapaswa kusaidiana bila kuangalia hali zetu au nchi zetu. Leo niko Tanzania, nimepokelewa kwa moyo wa upendo. Nawashukuru sana, napenda nchi yenu,” amesema Kalish.
Akizungumza kuhusu ujio huo, Rais wa New Life Foundation, Askofu Glorious Shoo amesema, ziara ya Kalish inalenga kuangalia namna ya kushirikiana katika kuwasaidia watoto kutoka familia zisizo na uwezo.
“Wamevutiwa na kazi tunayofanya. Tayari wameshatembelea baadhi ya nyumba zenye uhitaji mkubwa na tunajadili namna ya kushirikiana kuiboresha jamii, hususan kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu,” amesema Askofu Shoo.
New Life Foundation ni taasisi inayohudumia watoto wa Kitanzania wanaotoka kwenye mazingira hatarishi, ikiwapatia elimu, makazi na huduma za msingi za kijamii. Ziara ya Kalish inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya taasisi hiyo na wadau wa kimataifa.