Kiungo Simba arejesha majeshi Mashujaa FC

WAKATI fagio likiendelea kupitishwa Simba, kiungo wa zamani wa Mashujaa, Omary Omary amerudishwa alipotoka kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi hicho.

Kiungo huyo mshambuliaji tangu amesajiliwa na timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili, amekosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini hapo na chanzo cha kuaminika kutoka Simba kimeliambia Mwanaspoti, kiungo huyo hatakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao na wamefanya uamuzi wa kumtoa kwa mkopo.

“Omary ni miongoni mwa nyota ambao wanatolewa kwa mkopo kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya timu yetu akishindwa kuonyesha ushindani kwenye nafasi anayocheza hivyo tunamwondoa kupisha nyota wengine,” kilisema chanzo huku klabu ya Simba jana mchana ikithibitisha taarifa hizo.

Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta mchezaji huyo ambaye alithibitisha taarifa hizo ni za kweli na yeye ndiye aliyeomba kurudi Mashujaa baada ya kuona hana nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

“Taarifa za mimi kutolewa kwa mkopo ni za kweli na natarajia kurudi Mashujaa kama mambo yataenda vizuri, sikupata nafasi ya kuonyesha bado naamini nina nafasi ya kufanya vizuri kwenye timu nitakayopenda,” alisema na kuongeza.

“Ushindani ulikuwa ni mkubwa na nilikuwa kwenye timu ambayo ina presha ya matokeo huku ikiwa na malengo makubwa ya kutwaa mataji nafikiri ni muda sahihi wa mimi kurudi kujaribu maisha mengine naamini nina nafasi ya kufanya makubwa zaidi.”

Mbali na Omary, Simba ipo kwenye mchakato na timu nyingine kwa ajili ya kupeleka wachezaji wao kwa mkopo ambao ni Edwin Balua anayetajwa kupelekwa Enosis Athletic Union ya Cyprus, Valentino Mashaka huku Fabrice Ngoma, Valentino Nouma na Kelvin Kijiri wakitimkia timu nyingine baada ya kumalizana.

Related Posts