Dar es Salaam. Baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutoa vibali 10 vya ujenzi wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari (CNG), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kampuni zilizopewa vibali hivyo tayari zimeanza ujenzi.
Vibali hivyo kwa mujibu wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025/26, Ewura ilivitoa hadi kufikia Aprili, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Julai 12, 2025 Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Petroli, Emmanuel Gilbert amesema kwa sasa vituo saba vinafanya kazi, ambavyo vilivyopo ni Uwanja wa Ndege, Tazara, TOT-Tabata (viwili), Ubungo na Barabara ya Sam Nujoma (viwili).
Amesema vituo vipya ambavyo ujenzi unaendelea ni vya kampuni ya mafuta ya Puma inayovijenga vitatu katika maeneo ya Ubungo External, Tegeta na Tangi Bovu.
Gilbert amesema vituo vingine vinajengwa na kampuni ya Energo Tanzania (barabara ya Coca Cola), kampuni ya BQ (barabara ya Goba), kampuni ya TANHEALTH (Mbezi Beach), kampuni ya TAQA Dalbit (barabara ya Bagamoyo).
Vituo vingine amesema vitajengwa Kigamboni, Kibada na Kampuni ya Anric Energy, huku Kampuni ya NAT Energy itajenga kituo Tabata. Pia kampuni ya Victoria itajenga kituo eneo la Kipawa.
“Katika kuongeza wigo wa utoaji huduma tumeagiza vituo hamishika sita vya gesi vyenye thamani ya Sh8.5 bilioni, hapa tupo kwenye hatua za kusaini mkataba. Tukishasaini utekelezaji utaanza baada ya miezi sita kuanzia muda wa kusaini mkataba wenyewe,” amesema.
Amesema vituo hivyo sita, vitatu vitakuwa Dar es Salaam eneo la Msasani, Mikocheni na Ilala Bungoni, kitalu cha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Gilbert amesema vituo vingine vitatu vitakuwa mkoani Morogoro na Dodoma.
“Tukikamilisha mradi wa vituo hivi sita maana yake mtu atakuwa na uwezo wa kutoka na gari kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma na atapata gesi asilia bila shida,” amesema.
Akizungumzia utendaji wa kituo mama cha gesi eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kwa siku magari 600 na bajaji zaidi ya 600 zinahudumiwa.
Amesema magari yanayotumia gesi ni zaidi ya 5,000, huku bajaji zikiwa nyingi kupita kiwacho hicho cha magari.
Meshack Japhet, mkazi wa Kimara anayetumia gesi kwenye gari lake amasema kwa sasa upatikanaji wa nishati hiyo umekuwa nafuu tofauti na miezi ya nyuma.
“Sasa unaweza kwenda kujaza gesi na kuondoka kwa muda mfupi, hii kwetu ni faida kwa sababu tunatumia muda mrefu kutafufa fedha, tofauti na si kusubiri kujaza gesi,” amesema.
Kwa mujibu wa Ewura matumizi ya gesi asilia huokoa gharama kwa zaidi ya asilimia 50 ya gharama anazotumia mtu kwenye dizeli na petroli.
Kwa mfano, mtungi wa kilo 15 wa CNG hujazwa kwa Sh23,000 na hutembea wastani wa kilomita 250 kwa gari aina ya Toyota IST ambazo zingegharimu wastani wa Sh80,000 kwa mafuta.