Dodoma. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amesema kutoridhisha kwa hali ya utunzaji wa kumbukumbu dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya na hospitali, kunatatiza usambazaji wa dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD) na kutoa mwanya wa matumizi yasiyo sahihi na wizi.
Dk Mpango amesema hayo leo Jumamosi Julai 12, 2025 wakati akifungua mkutano wa mwaka wa waganga wakuu wa mikoa na halmashauri jijini Dodoma.
Akizungumza Dk Mpango, amesema hali ya utunzaji wa kumbukumbu dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya bado hairidhishi na kuwa hospitali na vituo vya afya bado havina utaratibu mzuri unaoonyesha matumizi sahihi ikiwemo bakaa ya vifaa hivyo.
“Na hali hii inatatiza usambazaji wa dawa kutoka MSD na kutoa mwanya wa matumizi yasiyo sahihi na wizi kwa hiyo nawaagiza kuimarisha eneo la utunzaji wa kumbukumbu, ili kuleta ufanisi katika eneo la utunzaji wa dawa na vifaa tiba na kuepuka kupotea,” amesema.
Amesema jambo jingine ni kutopatikana kwa dawa muhimu katika hospitali na vituo vya afya ngazi ya tatu, hasa dawa za magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari na magonjwa ya moyo.
“Na pendekezo langu kwa Wizara ya Afya nawaomba mpitie upya mfumo wa utoaji wa dawa, ili kuruhusu dawa hizo kupatikana katika ngazi msingi na huduma za kliniki zinazotembea,” amesema.
Aidha, Dk Mpango amesisitiza elimu sahihi ya dawa hasa za maumivu na antibayotiki ambazo zikitumiwa vibaya madhara yake ni makubwa ambapo inasababisha usugu wa vimelea, kuathiri moyo, figo na ini.
“Ninawataka kulipa kipaumbele jambo hili kwa kuongeza juhudi za utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya dawa dhidi ya jamii yetu, kutambua na kuepuka matumizi holela ya dawa hizo,” amesema.
Dk Mpango amesema pia udaktari unaongozwa na kiapo cha maadili kinachowataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia miiko ya maadili na kuwa kama wasimamizi wa utoaji wa huduma kwenye maeneo, amewataka kusimamia kwa karibu utekelezaji wa kiapo hicho.
“Hii ni katika kuwahakikishia wananchi huduma bora, muendelee kushirikiana na Chama cha Madaktari na msisite kuchukua hatua kwa wanaobainika kuvunja viapo vyao, lakini bila kuonea ama kufitini daktari yoyote wa afya,” amesema.
Aidha, amesema wamepokea changamoto za madaktari hao na kuwa mawaziri wanaohusika na afya watapelekewa risala zao ili wafanyie kazi changamoto hizo, na kuwapelekea majibu viongozi wao ambayo pia atayapeleka kwa Rais Samia Suluhu Samia.
Awali, akiwa katika banda la MSD, Dk Mpango amesema wakati alipotembelea bohari hiyo alikuta hali ilikuwa ngumu ambapo kulikuwa na shida katika uwekaji wa kumbukumbu na ununuzi wa dawa na vifaa tiba lakini hivi sasa zimefanyiwa kazi.
“Ninachotaka changamoto zote zilizokuwepo ziondoke, wizi wa dawa ukome, wale wengine waliokuwa wanashirikiana na taasisi za mtu mmoja mmoja halafu dawa zinaishia kule kwa watu binafsi, mhakikishe wanaisha,” amesema.
Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema Serikali kupitia Tamisemi, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeandaa mpango elekezi wa uimarishaji uwezo wa kufanya na kutumia tafiti za kiutekelezaji katika kuboresha huduma za afya ngazi ya msingi kwa mwaka 2025 hadi 2030.
“Mpango huu lengo kuu ni kutoa mwelekeo kwa watumishi wa afya ngazi ya msingi kufanya tafiti na kutumia matokeo ya tafiti katika kutatua changamoto na kuboresha utoaji huduma bora za afya nchini,” amesema.
Pia amesema umeandaliwa mpango wa mafunzo kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya nchini ambao utawapa stadi za kiuongozi, kuwaimarisha kiuzalendo, na kifikra katika kuwahudumia Watanzania katika kila kona ya nchi.

Akisoma risala ya waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa, Dk Best Magoma ameshauri Serikali kuangalia uwezekano wa kutenga wa fedha za bidhaa za afya kupitia MSD ili kugharamia matibabu ya magonjwa ya milipuko kwa sababu kwa sasa wanatumia sehemu ya bajeti ya vituo, hivyo kuathiri ustahimilivu na utendaji wa vituo.
Pia, ametaka sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa zijengewe uwezo na taasisi za utafiti kama vile Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu – NIMR, Taasisi ya Afya ya Ifakara ili zifanye tafiti za kubainia visababishi vya vifo vya watoto wachanga pamoja na uzazi kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya maeneo husika.
Kuhusu suala la ajira, Dk Magoma amesema wanapendekeza kuendelea kuajiri watumishi wapya kwa kuzingatia mahitaji ya ikama na kuwajenga uwezo ili kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma bora.
Aidha, wamependekeza kuwepo mfumo wa mafunzo endelevu na usimamizi kwa waganga wakuu, waganga wafawidhi, maofisa ustawi wa jamii na lishe ili kuendelea kuwajenga uwezo.
Dk Magoma amesema pia kuwezesha waganga wafawidhi wa ngazi zote kuwa na posho za madaraka hatua ambayo itaongeza motisha.
Pia, wameshauri Serikali kuangalia upya mfumo wa utoaji wa fedha kwa wadau ili kuhakikisha fedha zinafika kwa wakati na kuongeza ufanisi.
Amesema zitengwe fedha za ununuzi wa vifaa kwa watu wenye mahitaji maalum kama vile fimbo nyeupe na mafuta kwa albino na kuwe na mpango wa motosha kwa watumishi wanaofanyakazi katika mazingira magumu.
Akijibu changamoto za madaktari, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema wameshaanza kufanyia kazi suala la posho ya madaraka kwa madaktari.
Kuwajengea uwezo viongozi kwenye sekta ya afya, amesema wameingia makubaliano Shirika la Afya Duniani (WHO) na Chuo Kikuu cha Havard wataanza kupeleka mafunzo kwa viongozi hao.
Kwa upande wa kugharamia magonjwa wa malipuko, Mhagama amesema wamekubaliana na wafadhili katika Mfuko wa Kupambana na Magonjwa ya Mlipuko (Pandemic fund) wamejipanga kwenye bajeti ya 2025/26 kuimarisha huduma za dharura katika mikoa yote Tanzania.
Naye Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Antony Mwandamaka ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa wanafikia dira ya Taifa ya afya bora kwa wote huku akipongeza mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) Tanzania, Dk Garlbert Fedjo amesema nchi nyingi za Afrika kwa sasa zinakusanya rasilimali kwa ajili kufanya tafiti na kuimarisha kinga kwenye magonjwa kama vile malaria na kwamba wanajivunia kuona Tanzania kwa mwaka ujao imejidhatiti kuimarisha upatikanaji wa dawa.
Amesema kuwa mabadiliko ya sera za wahisani yawaamshe kutafuta suluhisho kwenye nchi kwa kuhakikisha kila mkoa na wilaya na kila shilingi inayotolewa inatumika kwa kipaumbele kilichokusudiwa na kuondokana na matumizi yasiyo na tija.
Mwenyekiti wa Wadau wa Afya, Majaliwa Marwa amesema ni muhimu Serikali kuhakikisha wataalamu wa afya ikiwamo wauguzi wanakuwepo wa kutosha katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuondoa upungufu uliopo katika kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa ngazi ya afya ya msingi na rufaa.
Amesema zaidi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii 9,000 wamehitimu katika vyuo mbalimbali na bado hawajaajiriwa kwenye jamii na kuishauri Serikali kupitia mamlaka za Serikali za Mitaa kuja na mbinu endelevu ya kuwezesha uwepo wa wahudumu hao.
“Wadau wa maendeleo wanataka kuona sekta ya afya inafanikiwa kwa kutoa huduma bora na tunaihakikishia Serikali kuendelea kusaidia katika mpango wa miaka mitano ujao wa sita katika sekta ya afya,”amesema.
Amesema wanatumaini kuwa kupitia mpango huo changamoto za sekta ya afya zitatatuliwa na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utafanikiwa.