Polisi yamshikilia kigogo wa Chadema, wenyewe wasema…

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania linamshikilia Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Brenda Rupia kwa mahojiano.

Hatua ya kuhojiwa kwake, inatokana na kile kilichoelezwa na taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa usiku wa leo Jumamosi, Julai 12, 2025 na Msemaji wa Jeshi hilo kuuwa anatuhumiwa kutoa taarifa za uongo na uchochezi.

Awali, taarifa ya kukamatwa kwa Brenda ilianza kwa kusambaa katika mitandao ya kijamii ikieleza amekamatiwa mpaka wa Namanga, alikokuwa akifanya utaratibu wa safari ya kwenda nchini Kenya.

Taarifa hiyo ilieleza Brenda amekamatwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji, wamemnyang’anya hati yake ya kusafiria na amekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.

“Maofisa wa Uhamiaji wanasema kwamba wamepewa maelekezo kwamba Viongozi wa Chadema hawatakiwi kutoka nje ya mipaka ya Tanzania hivyo wamemnyang’anya hati yake ya kusafiri,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo, imeeleza kiongozi huyo amekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi kwa OCCID wa Namanga na sasa wanataka kumsafirisha kumpeleka Dar es salaam.

Kabla ya Polisi kuthibitisha kumshikilia, Chadema kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje na Diaspora, John Kitoka alitoa taarifa kwa umma akidai kuwa Brenda amezuiwa kuingia nchini Kenya na sasa anashikiliwa na mamlaka katika mpaka huo wa Namanga.

Taarifa hiyo imedai kuwa Brenda alikuwa safarini kuelekea Nairobi kwa ajili ya kikao kilichopangwa kabla ya kusafiri kwenda Munich, Ujerumani, ambapo alitarajiwa kushiriki kwenye mafunzo kuhusu demokrasia na uchaguzi.

“Tunapenda kuutaarifu umma leo Jumamosi Julai 12, 2025, Mkurugenzi wetu wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia amezuiwa kuingia nchini Kenya na kwa sasa anashikiliwa na mamlaka katika mpaka wa Namanga.”

“Tumepokea taarifa za kuaminika kuwa mamlaka zimepanga kumrudisha kwa nguvu Dar es Salaam,” imedai taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeeleza tukio hilo si la kwanza viongozi wa Chadema.

Awali  Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa alizuiwa kusafiri nje ya nchi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Chadema, Godbless Lema alinyimwa  haki ya kusafiri kimataifa.

“Chadema tunalaani matendo haya yanayoendelea kuwakandamiza viongozi wa kisiasa wa chama ambayo yanakusudia kuwanyamazisha na kuwazuia kushiriki katika majukwaa ya kidemokrasia ya kikanda na kimataifa,” imesema.

“Tunataka Serikali imuachie mara moja bila masharti yoyote na kuheshimu haki yake ya kikatiba ya uhuru wa kusafiri kushiriki shughuli za kisiasa,” imeeleza taarifa hiyo.

Related Posts