HADI kufikia Ijumaa usiku, taarifa zilibainisha Simba ilikuwa kwenye mazingira mazuri ya kummiliki kiungo Balla Moussa Conté kutoka CS Sfaxien ya Tunisia baada ya kufikia makubaliano ya kumpa mkataba wa miaka miwili, lakini ghafla, Jumamosi asubuhi likaibuka jambo jipya.
Kilichotokea ni Yanga imeingilia kati mazima na inabainishwa imemaliza dili moja kwa moja kwa kumpa mkataba wa miaka miwili, hivyo kufanya kiungo huyo kuleta balaa mitaa ya Kariakoo akizichonganisha klabu hizo kongwe za soka hapa nchini.
Kwa mujibu wa Transfermarkt, tovuti inayohusika na masuala mbalimbali ya kisoka ikiwemo thamani za wachezaji, inaonyesha thamani ya kiungo huyo ni Euro 550,000 ambazo ni sawa na Sh1.7 bilioni za Kitanzania.
Conte amekuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo wa Sfaxien na ni chaguo la kwanza la timu hiyo iliyoishia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024-2025.
Ijumaa ya Julai 11, 2025, taarifa zinabainisha Simba ilifikia makubaliano ya kumsajili kiungo huyo wa ulinzi raia wa Guinea mwenye umri wa miaka 21 ambaye ana mkataba wa mwaka mmoja na Sfaxien unaofikia tamati 2026.
Kabla ya kufikia makubaliano hayo, Simba ilishtushwa na taarifa za Yanga kuvamia dili hilo kibabe na inakaribia kumchukua kiungo huyo.
Taarifa hizo zikamfikia Kocha wa Simba, Fadlu Davids ambaye aliinua simu na kutaka kujiridhisha, kupitia kipa wa kikosi hicho, Moussa Camara ambaye anacheza timu moja ya taifa na Conte kama kiungo huyo kweli ameshawaponyoka.
Baada ya Fadlu kuambiwa bado Sfaxien haijakubaliana na Yanga kumaliza dili hilo, kocha huyo Msauzi alimuwahi tajiri wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ na kumtaka aingilie kati na kupigania saini hiyo.
MO hakutaka kupoteza muda na kumuangusha kocha huyo ambaye amemfanyia kazi kubwa msimu uliomalizika, akatangaza dau la kufuru.
“Tuliona tunapigiwa simu na kuambiwa bosi mkubwa wa Simba anataka kuongea na sisi, tukasubiri na kweli akapiga, tutaongea na akataka tumuunganishe bosi wa Sfaxien,” alisema mmoja wa watu wanaomsimamia Conte na kuongeza.
“Tuliongea vizuri, mwisho wa siku tukawaacha wao klabu mbili wamalizane.”
Wakati hali ikiwa hivyo upande wa Simba, jana mwakilishi huyo wa Conte alizungumza tena na Mwanaspoti na kusema Yanga ndiyo iliyofikia pazuri na Sfaxien juu ya kumsajili mchezaji wao.
Mtu huyo alisisitiza, wakati Simba ikiwa ndiyo kwenye nafasi nzuri ya kumchukua Conte, Yanga wakaenda haraka kumaliza dili hilo, hivyo hadi kufikia sasa anachofahamu mchezaji wao atatua Tanzania kwa ajili ya kujiunga na mabingwa hao wanaomiliki mataji matano kwa msimu wa 2024-2025 ambayo ni Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Simba ilimuhitaji Conte ikiwa ni sehemu ya kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao baada ya kuwapa mkono wa kwaheri baadhi ya wachezaji wake wakiwemo wanaocheza eneo la kiungo mkabaji raia wa kigeni, Augustine Okejepha na Fabrice Ngoma, huku Debora Mavambo akitajwa kuwa njiani kwenda Singida Black Stars.
Kuondoka kwa wachezaji hao, kunatoa mwanya kwa Simba kusaka wengine wa kuziba nafasi hizo, hivyo Conte alikuwa ni mtu sahihi.
Mbali na nyota wa kimataifa walioondoka, eneo la kiungo mkabaji kwa sasa Simba wamebaki wazawa, Yusuph Kagoma aliyekuwa mhimili mkubwa wa timu hiyo msimu uliomalizika. Mwingine ni Mzamiru Yassin ambaye hakuwa na nafasi kubwa ya kucheza kufuatia muda mwingi kuuguza majeraha.
Kwa upande wa Yanga, eneo hilo la kiungo cha chini lina Khalid Aucho ambaye ameongeza mkataba wa mwaka mmoja, Duke Abuya na Mudathir Yanga ambao wote wamejiwekea ufalme wao kikosi cha kwanza hali iliyofanya msimu uliomalizika Jonas Mkude, Aziz Andabwile na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kukaa sana benchi. Kwa mantiki hiyo, kiungo huyo kama akithibitishwa rasmi kwamba ni mali ya Yanga, ana kazi kubwa ya kufanya mbele ya viungo anaowakuta.
Katika msimu uliomalizika, Conte amecheza mechi 23 za Ligi Kuu ya Tunisia akiwa na kikosi cha Sfaxien huku akionyeshwa kadi saba za njano.
Pia amecheza mechi sita za Kombe la Shirikisho Afrika zikiwemo mbili za hatua ya makundi dhidi ya Simba. Kiungo huyo pia amecheza mechi mbili za Kombe la Klabu Bingwa kwa Nchi za Kiarabu.
Kiujumla, Conte amecheza idadi ya mechi 34 za Ligi Kuu ya Tunisia akiwa na kikosi cha Sfaxien.