Hoja saba zilizoibuliwa ziara ya siku 30 za ACT Wazalendo

Tanga/Lindi. Siku 30 za ziara ya Chama cha ACT Wazalendo, zimetamatika huku hoja za umaskini, hadhi ya Bunge, ahadi kwa Jeshi la Polisi, zikibeba uzito.

Kwa mujibu wa viongozi wa chama hicho, hoja hizo ndiyo msingi wa kwa nini wanashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, licha ya kile wanachosema kuna changamoto za kisheria ndani yake.

Katika ziara hiyo, iliyopewa jina la Operesheni Majimaji Linda Kura, imehusisha mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, Tabora, Katavi, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Msingi wa ziara hiyo ni kuhamasisha wananchi wajitokeze kupiga kura kwa kuwa ndilo jukwaa litakalowawezesha kuamua kiongozi wanayemtaka na hatimaye kufikia maendeleo stahiki.

Akiwa mkoani Shinyanga, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alisema ili kupatikana amani na utulivu nchini, Serikali haina budi kuzingatia utendaji haki kwa makundi mbalimbali ya wananchi.

Kauli ya Dorothy, inajibu kilichoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Kanisa la Arise and Shine, katika hotuba yake, aliposisitiza kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu nchini.

Wakati Dorothy akiyasema hayo, mtia nia ya ubunge katika Jimbo la Shinyanga kupitia chama hicho, Emmanuel Ntobi alisema jawabu la changamoto zote za haki nchini, litapatikana kwa wananchi kufanya uamuzi wa kubadilisha watawala.

Katika hotuba yake, Dorothy amerejea kauli ya Rais Samia kwenye uzinduzi wa kanisa hilo, alipotaka amani na utulivu, akisema yote hayo yatapatikana iwapo haki itazingatiwa.

“Sisi tunamwambia Rais Samia, amani haitakuwepo, wala utulivu bila haki. Haki lazima ijengeke na ionekane imejengeka. Ili kuwepo amani lazima kutendwe haki,” alisema.

Ntobi alisema jawabu la changamoto zote za haki na mambo mengine ni wananchi kufanya uamuzi wa kubadili viongozi na kutoa nafasi kwa wagombea wanaotokana na ACT Wazalendo.

Kada huyo ambaye pia ni naibu waziri kivuli wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, amegusia aliyoyafanya alipokuwa Diwani wa Ngokolo mkoani humo, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara na huduma, ingawa alikabiliwa na vikwazo lukuki.

Alisema ndiyo maana amehama Chadema ambayo imejitenga kushiriki uchaguzi, amehamia ACT Wazalendo kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.

Alitumia jukwaa hilo, kueleza Tanzania kwa sasa inapita nyakati ngumu za kisiasa kutokana na mgawanyiko wa wanaokubali kushiriki uchaguzi, wanaopanga kuuzuia na wasioelewa lolote.

“Hawa wasioelewa wanaona siasa ni ya wanasiasa wakati ndiyo inayotupangia kila kitu. Kwa hiyo siasa ni kwa ajili ya kila mtu wa kila chama,” alieleza.

Makamu mwenyekiti wa chama hicho bara, Issihaka Mchinjita alishangazwa Mkoa wa Shinyanga kuwa wa nne kwa kuchangia katika Pato la Taifa, mchango wake ni Sh7.5 trilioni, ikiwa chini ya mikoa ya Mbeya, Mwanza na unaoongoza ni Dar es Salaam. Lakini wananchi wake ni miongoni mwa wanaoishi kwenye mstari wa umaskini.

“Kwa hiyo mchango wenu katika Pato la Taifa ni mkubwa lakini ninyi ni kati ya watu maskini sana.”

Hatua ya kuishi chini ya mstari wa umaskini, alisema inamaanisha watu hao hawana uwezo wa kupata Sh1,700 kwa siku. Na wastani wake ni asilimia 30 ya wakazi wa mkoa huo.

Akihutubia mkutano wa hadhara mkoani Tabora, kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliwataka Watanzania kuwa makini na watu wanaosaka ubunge wakiwamo wachekeshaji, wasanii na watangazaji.

“Wamelidogosha Bunge kwamba limekuwa eneo la machawa au la uchekeshaji au mtu yeyote anayetaka kwenda. Bunge linatunga sheria, linaisimamia Serikali na ndilo linalowawakilisha watu.”

“Ukilifanyia utani Bunge, utakuwa umefanya utani uhai wa Taifa ili kuhakikisha mhimili huu haufanyiwi utani watu wa Tabora pamoja na machungu mliyonayo, hasira mlizonazo au kukata tamaa pigeni moyo konde twendeni kwenye uchaguzi,” alisema Zitto.

Uchaguzi silaha ya mapambano

Ziara hiyo pia imetumika kama jukwaa la chama hicho kueleza sababu za kuamua kushiriki uchaguzi.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Issihaka Mchinjita akiwa mkoani Kigoma, alisema uamuzi wao wa kushiriki mchakato huo unalenga kuongoza mapambano ya haki na thamani ya kura ya Mtanzania.

Kwa upande wa Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu alisema wanaingia kwenye mchakato huo, kwa sababu uzoefu unaonyesha hakuna mafanikio yaliyowahi kupatikana kwa kususia uchaguzi.

Alieleza hata wazee wa zamani walipambana bila kuisusia Serikali ya kikoloni na matunda yake ndiyo uhuru unaoshuhudiwa sasa.

Katika hoja hiyohiyo, Zitto alisema ACT Wazalendo kinashiriki uchaguzi mkuu kwa masilahi ya Watanzania hivyo, aliwataka wananchi kushiriki mchakato pasipo kujali yaliyojitokeza mwaka 2020 na 2024.

Hoja ndio ilitawala karibu maeneo yote waliopita kuzungumza katika mikutano ya ndani na hadhara iliyofanyika kwa siku 15 katika mikoa ya Tabora, Mbeya, Katavi, Ruvuma, Rukwa, Mtwara, Lindi na Pwani.

Alisema chama ACT Wazalendo, kinawapenda na kuwajali Watanzania na viongozi wake wanaamini nguvu ya wananchi kwenye upigaji kura ndio itakayoitoa CCM madarakani.

Ukiondoa hoja hizo, suala jingine lililochukua nafasi ni umaskini uliotawala katika mikoa mbalimbali ikiwemo ya Katavi na Tabora, licha maeneo hayo kuwa na rasilimali za kutosha za kuwezesha kuinua uchumi wao.

Ukiachana na Tabora na Katavi pia chama hicho, kiliitaja mikoa ya Mtwara na Lindi kwamba licha ya kubarikiwa rasilimali za kutosha ikiwemo gesi na bandari lakini bado wananchi wake wanaishi katika hali ya umaskini.

ACT Wazalendo kilisema kikifanikiwa kushika madaraka au kuwa wabunge na madiwani wa kutosha kitahakikisha kinafutafuta ushuru wa mazao ili kuleta ahueni kwa wakulima.

Kimesema kisiposhika dola kitawatumia madiwani na wabunge watakaopatikana ili kusukuma ajenda itakayowanufaisha wakulima wote nchini.

“Ushuru wa mazao unapaswa kuwa sifuri, najua kuna watu watauliza sasa mkifuta wa halmashauri watapataje fedha? ACT Wazalendo tuna timu ya wataalamu iliyofanya utafiti,” alieleza Zitto.

Katika ziara hiyo, Chama cha ACT Wazalendo, kimesema kitaendelea kupigania mradi wa Liganga na Mchuchuma uanze kazi ambapo utakaozalisha mapato ya Sh1.3 trilioni.

“Ajira za vijana hakuna kwa sababu bidhaa za msingi za viwandani zinatokana na chuma ambacho bila makaa ya mawe huwezi kukiyeyusha,” alieleza.

Akiwa mikoa ya Lindi na Mtwara inayosifika kwa zao la korosho, Zitto aliwaambia wananchi wa mikoa hiyo ACT Wazalendo ndio chama pekee chenye majibu ya changamoto ya zao hilo linaloingiza fedha nyingi za kigeni.

“Newala na Tandahimba mnaongoza kwa kilimo cha korosho mwaka jana zao hili limeingiza matrilioni kwa maana hiyo wakulima wa zao hili mnaingiza mabilioni ya fedha.”

“Pamoja na wakulima kuingiza fedha zinazotokana na korosho bado wananchi wao wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo barabara ya kiwango cha lami inayodaiwa kujengwa kwa kusuasua,” alidai Zitto.

Baada ya ahadi ya magari aina ya Cruiser na nyumba ya ghorofa kwa kila askari Polisi iwapo ACT Wazalendo itashinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, kada wa chama hicho, Peter Madeleka aliahidi kutoa Sh10 milioni kwa askari atakayethibitika kutekeleza vema wajibu wake wa kulinda kura kwenye uchaguzi.

Aliiambatanisha ahadi hiyo na ufafanuzi wa utekelezwaji wa kuwapatia gari aina ya Land Cruiser na ghorofa kila askari iwapo chama hicho kitashinda, akisema watadhibiti mabilioni yanayopotea kila mwaka kufanikisha hilo.

Akiwa mkoani Tanga kuhitimisha ziara hiyo, Madeleka alisema; “Kwenye uchaguzi wa Oktoba kwa kuangalia mienendo ya polisi atakayetimiza wajibu wa kulinda kura ipasavyo mimi Madeleka nitampa Sh10 milioni.”

Alisema atawatumia wananchi kumpa taarifa za kazi ilivyofanywa na askari husika naye atamtunuku kiasi hicho cha fedha.

“Kwa hiyo kama mnanisikia na mnaona umuhimu timizeni wajibu wa kulinda kura kwa haki,” alisema Madeleka.

Ahadi nyingine, alisema iwapo chama hicho kitashinda uchaguzi kitahakikisha familia zote zilizopotelewa na watu wao zitalipwa fidia, huku waliokuwa na nafasi za kutimiza wajibu huo na hawakuutimiza wakipelekwa mahakamani.

Kuhusu ahadi ya Land Cruiser kwa kila Polisi, alisema watu wanadhani mzaha lakini ni uhalisia kwa kuwa chama hicho kitadhibiti upotevu wa fedha, kama unaotajwa kwenye ripoti mbalimbali za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).

“Nayasema haya ili mpate hasira na kulinda kura na mtashirikiana na wananchi,” alisema.​​​​​​

Related Posts