EU yazindua programu ya Afrika, Ulaya kubadilishana utamaduni

Unguja. Umoja wa Ulaya (EU), umesema utaendelea kushirikiana na Afrika katika kuwawezesha wasanii wa mabara hayo mawili kuongeza ufanisi katika kazi zao za sanaa na utamaduni.

Mtendaji Mkuu wa mradi wa ushirikiano ya kuwawezesha wasanii baina ya Afrika na Umoja wa Ulaya kutoka taasisi ya Goethe ya Afrika Kusini, kupitia masuala ya kiutamaduni, Philina Wittke, amesema ushirikiano huo unalenga kuwapa wasanii fursa zaidi za mafunzo, kubadilishana uzoefu, na kupata masoko mapya ya kazi zao.

“Tutahakikisha kuwa wasanii wanapata nyenzo na mazingira bora ya kuboresha kazi zao na kushiriki maonesho ya kimataifa yatakayoongeza mwonekano na thamani ya kazi zao,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo Julai 13, 2025 wakati wa kuzindua programu hiyo ya kubadilishana utamaduni kati ya Afrika na Ulaya ili kuwapa fursa wasanii wa mabara hayo mawili Mjini Unguja.

Kwa mujibu wa mtendaji mkuu huyo, EU inaamini sanaa ni daraja muhimu la kuimarisha uhusiano wa kimataifa, kukuza vipaji, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, amesema mpango huo pia ni sehemu ya juhudi za umoja huo kuimarisha diplomasia ya kitamaduni na kuleta maendeleo jumuishi kupitia sanaa, hasa kwa vijana na wanawake ambao wanawakilisha sehemu kubwa ya jamii za Afrika.

Naye Mkurugenzi wa Ten Studio ambayo inasaidia wasanii wachanga na walioendelea ya jijini Dar es salaam Tanzania, God Ramadhan amesema mradi huo una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha wanasaidia na kukuza kazi mbalimbali za sanaa.

Amesema Tanzania bara na Zanzibar kupitia mabaraza yake, zimekuwa zikiwaunga mkono wasanii kwa lengo la kukuza ajira za vijana kupitia sanaa na utamaduni.

Amesema ni matumaini yake kuwa mradi huo utawapa fursa na nguvu zaidi ya kutengeneza sanaa zao na kukuza wigo wa shughuli wanazozifanya kupitia sanaa na utamaduni.

Mkurugenzi wa Chuo cha Muziki (DCMA), Hilda Mohamed Alkanaan amesema hiyo ni fursa katika kukuza vipaji na kuwainua wasanii, lakini pia kwa nchi za Afrika kushirikiana wenyewe kwa wenyewe  kuendeleza shughuli za kisanii.

 Mtendaji Mkuu wa Zanzibar International Festival (ZIFF), Joseph Mwale amesema mara nyingi wamekuwa wakitumia bajeti kubwa kuleta wasanii kutoka nchi za nje, lakini kupitia programu hiyo itawasaidia kupunguza gharama.

Related Posts