Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanza rasmi mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge katika ngazi ya Taifa, kikiwataka wote watakaokosa nafasi kuwa watulivu, waaminifu na watiifu kwa chama.
Aidha, chama hicho kimeeleza kwamba hadi sasa hakuna mgombea yeyote aliyekatwa au kuenguliwa, kwa kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu majina ya wagombea utatolewa na Kamati Kuu ya CCM.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia taarifa zilizozagaa mitandaoni zikidai kwamba kuna wagombea waliokatwa katika ngazi ya mikoa na wilaya.
Akizungumza leo Jumapili Julai 13, 2025, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema mchakato wa awali wa ukusanyaji maoni kuhusu watiania umekamilika katika ngazi za kata, kamati za siasa za wilaya na za mikoa.
“Hapa makao makuu vikao vya ngazi ya kitaifa vimeanza rasmi. Zoezi hili limehamia makao makuu. Leo tumeanza na Sekretarieti ya CCM kwa kupokea taarifa kutoka mikoa mbalimbali ambayo tayari imewasilisha taarifa zake,” amesema Makalla.
Ametoa wito kwa watiania wote kuwa watulivu hadi Kamati Kuu itakapotoa uamuzi wa mwisho kuhusu majina yatakayopitishwa.
“Kwa utaratibu na mchakato ndani ya chama, hakuna mtu aliyeenguliwa au kukatwa. Nimeona (mitandaoni) watu wakiandika fulani kafyekwa, hayumo kwenye tatu bora… Naomba mtupelekee ujumbe; hakuna aliyeenguliwa, hakuna aliyekatwa, hakuna aliyefyekwa. Huo ni mchakato unaoendelea ndani ya chama chetu,” amesema.
Makalla amesema idadi ya waliotuma maombi ni kubwa na wote wana nia njema, lakini ni wachache tu watakaopata nafasi kutokana na viti vilivyopo.
Amewahakikishia kuwa wale watakaokosa nafasi wanaaminiwa kuwa wazalendo na wenye mapenzi kwa chama na kwamba, wataendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki kikamilifu katika kukijenga chama hata baada ya mchakato wa kura za maoni.
Amesema chama kinathamini na kutumia kila mwanachama kulingana na nafasi yake na wajibu wake. Amesema wapo waliotuma maombi ambao ni viongozi au wanashika dhamana nyingine na hata wasipopata nafasi za kugombea, wataendelea kutimiza majukumu yao kwa uaminifu.
“Kikubwa zaidi, mwanachama wa CCM atakuwa ametimiza haki yake ya kugombea. Lakini pia kama mwanachama kati ya wanachama milioni 13 wa CCM, naye ni sehemu ya jeshi la chama na ana wajibu wa kukipigania chama chake,” amesema Makalla.
Akijitolea mfano wa uzoefu wake
binafsi amesema, katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 aligombea ubunge Jimbo la Mvomero, akashinda kura za maoni kwa nafasi ya kwanza, lakini nafasi ile akapatiwa aliyeshika nafasi ya tatu.
Amesema licha ya hayo, alimuunga mkono mgombea aliyechaguliwa na chama ambaye ndiye mbunge aliyemaliza muda wake na hakuwahi kuonyesha malalamiko au chuki.
“Nilikaa kwa utulivu. Baada ya hapo niliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kisha Mwanza na sasa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo. Mimi ni mfano hai unaotembea kwa wale watakaokosa nafasi. Chama chetu kina hazina ya wanachama na majukumu mengi. Waige mfano wangu, sikuyumba, nilitulia, nilikipenda chama changu na hatimaye nikateuliwa kwenye nafasi nyingine,” amesema.
Makalla amewaomba wagombea wote kuwa watulivu hadi Kamati Kuu itakapokamilisha mchakato na kutangaza majina ya wagombea watakaoiwakilisha CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Amesisitiza pia kuwa mwakani chama kina uchaguzi wa ndani, wanachama watapata fursa nyingine ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.