Iringa. Wafanyabiashara wa Soko la Mashine Tatu katika Manispaa ya Iringa, ambao mali zao ziliungua usiku wa kuamkia Julai 12, 2025 wameiomba Serikali iwasaidie warejee kwenye shughuli zao za kiuchumi baada ya kupoteza kila kitu katika janga hilo.
Mwananchi Digital ambayo leo imefika sokoni hapo iliwakuta wafanyabiashara hao wakichambua mabaki ya sehemu y mali zao zilizoungua, huku baadhi yao wakilia kwa uchungu.
Wakizungumza katika kikao kilichowakutanisha na viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Iringa leo Jumapil Julai 13, 2025 sokoni hapo, wafanyabiashara hao wameshukuru kwa hatua na taratibu zinazochukuliwa na Serikali, hata hivyo wamesema changamoto kubwa iliyosalia ni ukosefu wa mitaji itakayowasaidia kurejea tena kwenye biashara zao sokoni hapo.
Elesia Luvanga, mfanyabiashara wa viungo sokoni hapo, amesema hatua ya kuhamishiwa kwenye masoko ya Zizi, Ngome, Ipogolo, Magari Mabovu na Mlandege itawasaidia kwa kiasi fulani, lakini haitakuwa na maana kama hawatapata bidhaa za kuanzia biashara zao.
Baadhi yao, wakiwa wamepiga magoti mbele ya viongozi wa Serikali ya mkoa, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan awasaidie kupata mitaji ili waweze kuanza upya maisha yao ya kibiashara.
“Nimefanya biashara pale miaka mingi, sijawahi kuona janga kama hili. Nimeliacha eneo nikiwa sina kitu zaidi ya mavumbi. Tunaomba Rais Samia atusaidie,” amesema Elesia.
Naye Nasra Said aliyesema amepoteza kila kitu, hajui ataanzia wapi hata kama atapatiwa kizimba eneo lingine.
Amesema moto huo umeharibu kabisa maisha yake ya kila siku na sasa haelewi aanzie wapi.
“Hata chakula cha watoto wangu hakina uhakika. Tunaomba msaada wa mtaji kutoka serikalini. Rais Samia tusaidie, wengine tunaishi na watoto yatima zaidi ya ishirini, watakula nini hawa?” amesema Nasra huku akilia na kuwaliza wenzake katika kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James akizungumza kwenye kikao hicho amesema Serikali inatambua maumivu yao na imeunda kamati ya maafa kuratibu hatua za muda mfupi na mrefu za kuwanusuru.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta kwa kushirikiana na Jeshi la Akiba na Kikosi cha Zimamoto, kuhakikisha eneo lililoungua linakuwa safi ifikapo Julai 16, 2025 ili maandalizi ya ujenzi au matumizi salama yaanze.
“Hili eneo linamilikiwa na Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania), lakini Serikali haitategemea hoja hiyo pekee. Tutashirikiana na taasisi hiyo kuhakikisha miundombinu ya muda inapatikana kwa waathirika wote,” amesema James.
Ametoa wito kwa taasisi binafsi na wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wafanyabiashara hao.
Amesisitiza kuwa huu si wakati wa kukata tamaa, bali wa kuchukua hatua za kweli kuinua walioyumba kiuchumi.
Kuhakikisha usalama wa masoko yote mkoani Iringa, James ameagiza masoko yote kufungwa kamera za ulinzi (CCTV) ili kudhibiti uhalifu na majanga ya moto.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Iringa, Musa Haruni amesema watafanya tathmini mpya ya makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara walioathirika.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa Bakwata Mkoa wa Iringa, Kibigili Said amesema wamepokea maelekezo ya Serikali kuhusu mpango wa muda na wapo kwenye hatua za kuhakikisha wafanyabiashara wanarejea sokoni haraka.
Aidha, imeelezwa kuwa mazungumzo yanaendelea kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhusu mpango wa kujenga jengo la kisasa katika eneo la Stendi Kuu ya zamani ili kutoa suluhisho la kudumu.
Mwenyekiti wa soko la Mashine Tatu, Jafari Sewando amesema Serikali imekuwa ya kwanza kuwafariji na hatua hiyo inaonyesha kuwa viongozi wanaguswa na mateso ya wananchi.
“Bado tunaamini Rais Samia ataendelea kuwa mama wa huruma kwa Watanzania wote,” amesema Sewando.
Moto huo uliounguza soko hilo umewaacha mamia ya familia bila chanzo cha kipato. Ingawa wengi hawajui mustakabali wao, matumaini yao yapo kwa Serikali, taasisi za fedha, mashirika ya misaada na watu binafsi kuwasaidia kurudisha ndoto zao kwa haraka.