Conte anaingia, Chama ndo hivyo tena!

YANGA imendelea na hesabu zake za kimafia kusuka kikosi chake na lile dili la kiungo wa shoka Moussa Bala Conte likitiki tu basi, litamng’oa staa wa maana ndani ya kikosi hicho kwa msimu ujao wa mashindano.

Yanga hadi jana ilikuwa ikiendelea kupigania saini ya Conte raia wa Guinea ambaye pia alikuwa anawaniwa na Simba ambao ndio walitangulia kumsaka kiungo huyo.

Conte alikuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu ya Sfaxien ya Tunisia ambayo ni kama ilikuwa inasubiri ofa tu ya kumuachia.

Hesabu za Yanga ni kwamba wanataka huduma ya Conte kwa akili ya kuboresha eneo la kiungo wa chini, kucheza sambamba na mkongwe Khalid Aucho au Mudathir Yahya.

Yanga pia inamtaka Conte ili kuanza kujiandaa na mazingira kama watamkosa Aucho ambaye msimu uliopita alikumbana na majeraha kwa nyakati tofauti.

Ujio wa Conte utalazimika kumuondoa staa mmoja wa kigeni ambapo hesabu hizo zimemuangukia Chama akitakiwa kumpisha kiungo huyo.

Chama amemaliza mkataba aliokuwa nao na klabu hiyo mwisho wa msimu huu akiitumikia Yanga kwa mwaka mmoja pekee, akitokea Simba, kama mchezaji huru.

Yanga ilikuwa ipambana na Chama kumshusha bei, akitaka dau ambalo viongozi wa klabu hiyo walishindwa kukubaliana naye huku mechi nyingi akiwa anatokea benchini.

Yanga inaona kwamba, eneo ambalo Chama anacheza endapo Mzambia huyo ataondolewa, bado litakuwa salama kwa kuwa Pacome Zouzoua analimudu sambamba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anatajwa kuwa kwenye hesabu za kumrudisha.

“Eneo ambalo anacheza Conte kuna mchezaji mmoja wa kigeni ambaye ni Aucho, lakini tumembakisha kwa mwaka mmoja zaidi ukiangalia anavyokwenda,” alisema mmoja wa mabosi wa Yanga na kuongeza;

“Msi-mu huu uliokwisha tulikuwa na changamoto kubwa kama ukimkosa Aucho unakosa mtu wa maana zaidi kucheza pale chini, unabaki na Mudathir pekee sasa haikuwa salama au wakati mwingine unamshusha Sure Boy (Abubakar Salum).

“Kule juu utaona kuna watu wengi, unalazimika kumuongezea mkataba kwa nguvu yoyote Pacome lakini una Chama unaangalia muda aliotumika, na athari hasi kama ukimkosa, unaona bado mtakuwa salama, haya kuna Feisal usisahau utaona namna tutakavyokuwa salama eneo hilo.”

Licha ya kuwa na vita kali kati ya Simba na Yanga kumwania, lakini Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba nyota huyo raia wa Guinea amedaiwa kusaini mkataba wa miaka miwili Jangwani.

Related Posts