Ayoub Lakred avunja ukimya | Mwanaspoti

SIKU chache tangu amalizane na Simba, kipa Ayoub Lakred aliyetua FUS Rabat ya Morocco, amevunja ukimya kwa kufichua kuwa, licha ya kuondoka Msimbazi, lakini klabu hiyo itaendelea kuwa moyoni mwake kwa namna alivyoishi nayo, huku akiitaja Yanga.

Lakred aliyeitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja ya kupata majeraha yaliyomweka nje kwa muda mrefu, licha ya kuendelea kulipwa na Simba licha ya kuletwa kwa Moussa Camara aliyemaliza msimu uliopita kwa kupata clean sheet 19 za Ligi Kuu na saba za Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Kipa huyo raia wa Morocco amemalizana na klabu hiyo na kurejea kwao baada ya kupata dili la kuitumikia timu aliyowahi kuitumikia ya FUS Rabat na akiwa huko amezungumza na Mwanaspoti na kukiri alivyoshindwa kujizuia kubaki na Simba moyoni mwake kutokana na kumbukumbu nyingi nzuri alizonazo wakati akicheza soka la kulipwa Tanzania.

Katika msimu wa mwisho Simba, Ayoub aliondolewa katika mfumo wa usajili baada ya kuumia na nadasi yake kuchukuliwa na Camara na kipa huyo amesema anajisikia faraja kuwa sehemu ya kikosi hicho kipindi chote alichoitumikia ikiwamo kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Simba sio timu tu, kiukweli kwangu ilikuwa familia. Nilihisi kuwa sehemu ya kitu kikubwa zaidi ya soka. Mashabiki walinionyesha mapenzi ya dhati, benchi la ufundi liliamini uwezo wangu na wachezaji wenzangu walinifanya nijihisi nyumbani,” alisema Ayoub.

Pia alisema amejifunza mambo mengi ikiwamo upinzani mkubwa baina ya Simba na Yanga na kwamba amegundua mashabiki wa soka wa Tanzania wanazipenda mno timu zao na huwa wanaumia zinapopoteza mbele ya wapinzani.

Ayoub alikuwa sehemu ya kikosi kilichopoteza kwa mabao 2-1 mbele ya Yanga katika mechi ya Dabi ya Kariakoo ya marudio ya msimu wa 2023-2024 iliyopigwa April 20 mwaka jana baada ya awali Simba kulambwa mabao 5-1 Novemba 5, 2023 ambapo langoni alisimama Aishi Manula.

Katika maisha yake ya Msimbazi mara alipotua kipa huyo alikuwa namba moja wa Wkundu hao, Ayoub alisema yalikuwa mzuri na yenye kumbukumbu nyingi nzuri hasa msimu wa 2023–24 chini ya kocha Abdelhak Benchikha.

Ndani ya msimu huo, Simba ilipenya Kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa nafasi ya pili nyuma ya ASEC Mimosas, huku ikizizidi kete Wydad Casablanca ya Morocco na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Hata hivyo, Simba iliishia hatua ya robo fainali kwa kutupwa nje na mabingwa wa kihistoria wa Ligi hiyo, Al Ahly kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-0, ilihali watani wao Yanga, iking’olewa kwa penalti 3-2 na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Ayoub, amekula kiapo akisema kuwa, licha ya kuondoka Simba ataendelea kufuatilia mwenendo wa timu hiyo ambayo msimu uliopita ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa chini ya kocha kijana, Fadlu Davids.

“Hii ni kazi yangu na lazima maisha yaendelee, lakini moyo wangu utabaki na Simba. Najua mashabiki wa Msimbazi wana moyo wa upendo. Nitakuwa mmoja wao kwa mbali, nikifuatilia kila hatua yao. Walinipa kitu ambacho si rahisi kukipata sehemu nyingine,” alisema Ayoub.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 30 amejiunga na FUS Rabat kwa mkataba wa miaka miwili akiwa mchezaji huru utakaomalizika Juni 30, 2027 ambapo katika usajili huo Ayoub imedaiwa amevuta Euro 400,000 ambazo ni zaidi ya sh 1.2 bilion.

Related Posts