TAARIFA mbalimbali zinaeleza kuwa kiungo wa Simba, Edwin Balua ametolewa kwa mkopo wa mwaka mmoja kwenda Enosis Union Athletic Paralimni FC ya Cyprus.
Makubaliano ya mkataba huo wa mkopo yana kipengele cha kumnunua moja kwa moja iwapo ataonyesha kiwango bora.
Timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo ina historia yake kwenye mashindano ya ndani na kimataifa, na msimu huu imejipanga kusajili kuhakikisha inafanya vizuri.
Kwa muda mrefu haijaonyesha ushindani kwenye mashindano ya ndani, kwani mwaka 2002 ilifika fainali ya mashindano ya Cypriot Cup.
Hivyo, imepita zaidi ya miaka 20 tangu timu hiyo iwe na mafanikio makubwa; imekuwa ikipanda na kushuka kati ya Daraja la Kwanza na la Pili.
Imejijengea heshima kama klabu ya mkoa inayoongoza kwa kukuza vipaji vya wachezaji, kama ilivyo Mtibwa Sugar kwa Tanzania.
Iliwahi kushiriki mashindano ya UEFA Intertoto Cup mwaka 2003, lakini haikufika mbali ikatolewa mapema.
Mashindano hayo yalikuwa ni njia mbadala kwa klabu vya daraja la kati Ulaya kupata nafasi ya kufuzu UEFA Cup (sasa Europa League), lakini yalifutwa baadaye na UEFA.