Maombi ya Chadema kumkataa Jaji kusikilizwa leo Mahakama Kuu

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo Jumatatu Julai 14, 2025  inatarajia kusikiliza maombi ya Chadema ya kumtaka Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama hicho, kujiondoa kwenye kesi hiyo.

Maombi hayo yanatarajiwa kusikilizwa wakati kesi ya msingi ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Julai 10, 2025, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Bodi ya Wadhamini wake waliosajiliwa kiliwasilisha maombi rasmi ya kumtaka Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi yake ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama, ajiondoe kwenye kesi hiyo.

Pia, chama hicho kilifungua shauri la maombi kikiiomba Mahakama hiyo, iondoe amri zake za zuio dhidi ya wadaiwa katika kesi hiyo, (Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu), kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama.

Siku hiyo wakati kesi ya msingi ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadaiwa, Mpale Mpoki aliieleza Mahakama kuwa wadaiwa hao (bodi ya wadhamini na katibu mkuu) wameandika barua ya kumtaka jaji huyo ajitoe katika kesi hiyo.

Wakili Mpoki alidai barua hiyo iliyoandikwa Juni 23, 2025 iliwasilishwa kwa Naibu Msajili Juni 24, 2025.

Kwa upande wake, wakili wa wadai, Shabani Marijani alidai walipata taarifa za kuwepo kwa barua hiyo ya wadaiwa kumkataa jaji siku hiyo  asubuhi.

Hivyo walidai  kwa kuwa suala la kumkataa jaji ni la kisheria, wanaomba ahirisho la muda wa kuipitia ili kuona kama kuna hoja huku akiiomba Mahakama iwape muda mfupi kwa kuwa shauri hilo linagusa masilahi ya umma.

Jaji Mwanga alikubaliana na hoja na maombi hayo na kupanga kusikiliza maombi ya wadaiwa kumtaka ajitoe katika kesi hiyo leo, ambayo kesi ya msingi pia itatajwa.

Shauri la maombi ya kuondoa amri za mahakama za zuio la wadaiwa kufanya shughuli za kisiasa na matumizi ya mali za umma nalo litatajwa leo Jumatatu.

Hata hivyo, kutokana na kuwepo maombi hayo, madai ya msingi ya wadai yamesimama kwa muda usiojulikana kusubiri mpaka maombi hayo yote yatakapotolewa uamuzi.

Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho taifa, Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Komu, ambao ni wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kutokea Zanzibar.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni bodi ya wadhamini wa Chadema, mdaiwa wa kwanza na katibu mkuu wa chama hicho ni mdaiwa wa pili.

Katika kesi hiyo ya madai ya mwaka 2025, wadai wanadai   kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo wanaomba Mahakama hiyo iamuru kwamba wadaiwa wamekiuka  katiba ya chama hicho na kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze kuzingatia sheria hiyo na katiba yake.

Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa  ni kinyume cha sheria na ni batili.

Amri nyingine wanazoziomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama, amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi adaiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.

Vilevile wanaiomba Mahakama iamuru, wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo  itaona inafaa kuzitoa.