PSPTB YANG’ARA SABASABA, YAKWAA NAFASI YA PILI KWA TAASISI ZA SERIKALI


Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imeibuka mshindi wa pili katika kundi la Taasisi za Serikali zilizoshiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Tuzo hiyo imetolewa kwa kutambua mchango wa PSPTB katika kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa weledi, yakiwemo uendeshaji wa mafunzo na mitihani ya kitaaluma, usajili na usimamizi wa mienendo na maadili ya wataalam wa ununuzi na ugavi pamoja na utoaji wa ushauri kwa serikali na sekta binafsi kuhusu masuala ya kitaaluma ya ununuzi na ugavi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano wa PSPTB, Bi. Shamim Mdee alisema ushindani katika kundi la Taasisi za Serikali ulikuwa mkubwa kutokana na wingi wa taasisi zilizoshiriki, lakini ushindi wao umetokana na maandalizi mazuri na ufanisi wa timu yao

“Siri ya ushindi wetu ni maandalizi ya kina yaliyolenga kutoa huduma bora kwa wageni waliotembelea banda letu. Tulihakikisha tunaelewa kwa undani huduma na bidhaa za PSPTB, tuliwasikiliza wateja kwa makini, tulivaa kwa nidhamu ya utumishi wa umma, na tuliandaa banda lenye mwonekano wa kuvutia na wa kipekee ulioonyesha namna rahisi ya kupata huduma zetu kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa Online Registration System,” alisema Bi. Shamim.

Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wa PSPTB, Bi. Shamim alitoa shukrani kwa Wizara ya Fedha kwa ushirikiano mkubwa waliopatiwa tangu maandalizi hadi kufanikisha ushiriki wao katika maonesho hayo.

“Tunawashukuru pia wadau wote waliotutembelea kwenye banda letu. Tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora na ya kiwango cha juu kwa wadau wa taaluma ya ununuzi na ugavi nchini,” aliongeza.

Maonesho ya 49 ya Sabasaba mwaka huu yamehusisha taasisi, mashirika, kampuni na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, yakilenga kukuza biashara na kuonyesha fursa mbalimbali zinazopatikana Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfred Mbanyi akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Bodi hiyo katika Banda la PSPTB katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 49 kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam

Related Posts