:::::::
Mjumbe Maalum wa Wanawake, Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika, Mh. Balozi Liberata Mulamula ameshiriki Mkutano wa Taasisi ya Maendeleo ya Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD) na Mkutano wa Umoja wa Afrika, (AU), uliohusisha viongozi mbalimbali huku akisisitiza Nchi hizo kusaini na kuridhia Mkataba wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana.
Balozi Mulamula amesisitiza hayo wakati akichangia hoja katika mkutano huo akiwa mjumbe mwakilishi maalumu wa wanawake wa Afrika, nafasi aliyochaguliwa mwaka huu.
Katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika, Tanzania imewakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo kwa niaba ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo ulifanyika Malabo, Equatorial Guinea, ukihitimishwa kwa maazimio ya dhamira ya dhati ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo kujenga Afrika iliyo huru kifedha na yenye ustawi.
Viongozi hao wa Afrika wameahidi kuunda ushirikiano wa mageuzi na kufungua mikakati ya pamoja ya uhamasishaji rasilimali ili kutimiza malengo kabambe ya Ajenda ya 2063
Mkutano huo, uliofunguliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Mhe. Mahmoud Ali Youssouf wenye kaulimbiu ‘PAMOJA – Working Together to Ignite Regional Integration ulisisitiza umuhimu wa kuwa na juhudi za pamoja katika kushughulikia suala la ufanisi, kujenga uwezo, na ushirikishwaji wa diaspora ya Afrika
Mkutano huo umehudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa AUDA-NEPAD, Bi. Nardos Bekele-Thomas na Wajumbe wengine kutoka Taasisi za Umoja wa Afrika, na Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda.
Pamoja na masuala mengine, vipaumbele muhimu vilivyotambuliwa ni kuoanisha mipango ya bara kuhusu uendelezaji wa viwanda, mabadiliko ya kidijitali, makabiliano ya mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda (RECs) na AUDA-NEPAD zilisititiza umuhimu wa kufanya shughuli zenye tija na matokeo hususani kutafuta fedha za ufadhili wa miradi ya kipaumbele zaidi ya 300 badala ya kuendelea na hulka ya kufanya mikutano kila mara.
Viongozi wamesisitiza juu ya utumiaji wa rasilimali za ndani, ushirikishwaji wa sekta binafsi, na uwezeshwaji wa wanawake kama moja ya vichocheo muhimu katika kufikia maendeleo endelevu. Aidha, viongozi walikazia kuwa suluhisho la matatizo yanalolikabili bara la Afrika ni jukumu la Waafrika wenyewe.
00000