Katika tukio la kushtua lililotokea leo jijini London, ndege aina ya Beech B200 Super King Air imeanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Southend.
Tukio hilo limenaswa kwenye video inayosambaa kwa kasi mitandaoni, ikionesha mlipuko mkubwa wa moto uliofuatia ajali hiyo. Mabaki ya ndege yaliteketea kwa moto huku moshi mzito ukifuka angani, na kuvuta huduma za dharura kufika haraka eneo la tukio.

Hadi sasa haijafahamika ni watu wangapi walikuwa ndani ya ndege hiyo, lakini kwa kawaida ndege ya aina hiyo hubeba hadi abiria 12. Ndege hiyo yenye injini mbili ilikuwa inatarajiwa kuanza safari kuelekea Lelystad, Uholanzi saa 9:45 alasiri.
Mashuhuda waliokuwepo uwanjani wameeleza kuwa tukio hilo lilikuwa la kusikitisha sana, huku wengine wakidai kuwa waliona wafanyakazi wa ndege hiyo wakiwapungia mikono abiria muda mfupi kabla ya ajali hiyo kutokea.
