Dar es Salaam. Leo katika mwendelezo wa mapitio ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Mahakama inahitimisha uchambuzi kuhusu hatia kwa waliohusika kutekeleza mauaji hayo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.
Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi) na Salim Mbalu alikuwa Koplo.
Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo wilayani Mtwara.
Katika sehemu iliyopita, Jaji Hamidu Mwanga kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, aliwatia hatiani washtakiwa katika kundi la tatu ambao ni Kalanje na Onyango.
Jaji Mwanga aliwatia hatiani kwa kanuni ya kisheria ya mtu wa mwisho kuonekana na mtu ambaye baadaye anapatikana amekufa na mtu huyo kushindwa kutoa maelezo ya mazingira ya kifo hicho na ushahidi wa mshtakiwa wa tano.
Sasa katika simulizi ya leo, Jaji Mwanga anaendelea na uchambuzi wa ushahidi unaounga mkono ushahidi wa mshtakiwa mwenza ili ukidhi sifa ya kisheria ya kuuzingatia katika kumtia hatiani mshtakiwa mwenza.
Ushahidi wa washtakiwa watatu
Kama ilivyoelezwa awali, kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa 5,23 na 25 Kalanje na Onyango walifika Kituo cha Polisi Mitengo Januari 5, 2025 (mchana), wakiwa na Mussa, mshtakiwa wa tano na Afande Mahembame.
Jaji akasema kulingana na ushahidi wao, waliomba chumba cha kumuhojia Mussa na walipewa kilichotumika kama stoo kisha waliomba kufuli na walimfungia marehemu ndani, kisha wakaondoka na funguo.
Baadaye usiku saa sita, Kalanje, Onyango, Afande Greyson Mahembe na mtu mwingine walifika kituoni hapo na machela, wakimwambia shahidi wa tano walikwenda kuchukua mgonjwa wao, lakini hakuwa na taarifa kuwepo kituoni.
Kwa mujibu wa Jaji, alimuona Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Mahembe na mtu mwingine wakimbeba mtu asiyeonesha kuwa hai juu ya machela.
Vilevile kuna ushahidi wa shahidi wa 17, Inspekta Adelina Lyakana kuwa Januari 5, 2022 saa 7:00 usiku katika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, alimwona Kalanje, Onyango na Mahembe wakiingia ofisini huku Mahembe akirudisha machela.
Pia, shahidi wa tatu, alieleza kuwa baada ya mshtakiwa wa tano kueleza tukio la Kituo cha Polisi Mitengo, Inspekta Msaidizi Mahembe aliwaonesha mahali ambako mwili wa marehemu ulitupwa, katika msitu wa Hiari.
Mahali hapo, ilipatikana iliyodhaniwa mbavu na mifupa ya miguu ya binadamu iliyothibitishwa katika ripoti ya shahidi wa tisa ambaye ni Mkemia wa Serikali.
Akaendelea kuchambua ushahidi huo, Jaji aliendelea kueleza kuwa, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba (DNA) kwa kulinganisha sampuli ya mate ya shahidi wa kwanza (mama wa marehemu), mifupa hiyo ilibainika ni ya Mussa.
“Kwa hiyo, matendo na mwenendo kama yalivyoelezwa na mashahidi hao yanatosha kuthibitisha ushahidi wa shahidi wa tano wa utetezi (mshtakiwa wa tano), hivyo yanastahili kuaminiwa na kuthibitisha kesi ya upande wa mashitaka.
“Mazingira hayo yote kwa pamoja yanaelekeza moja kwa moja kwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili kuwa ndio waliomuua Mussa Hamis Hamis,”alisema Jaji.
Utetezi wa kutokwenda kituoni ulivyotupwa
Jaji alisema kuna hoja nyingine ya utetezi kutoka kwa washtakiwa kwamba hawakwenda kabisa Kituo cha Polisi cha Mitengo kwa kuwa hawakutia saini kwenye daftari la mahudhurio la maofisa ambalo ni kielelezo PF187.
“Hiyo si hoja ya msingi inayoweza kuwanasua na hatia kama maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakisimamia kituo hicho, na kuwa na jukumu la kusimamia utendaji wa askari wa chini yao na taratibu za kazi kituoni hapo.”
“Walikuwa na ufahamu wa kuweka saini kwenye daftari hilo lakini walikwepa kwa makusudi. Hivyo hawawezi kuitumia kama kinga,”alisisitiza Jaji Mwanga.
“Kutokana na asili ya shughuli waliyokuwa wanatekeleza, walihitaji kuepuka kuacha ushahidi wa mahudhurio yao, hivyo hoja hiyo haitoi msaada wowote.
“Utetezi huo pia, unapingwa na ushahidi wa shahidi wa 23 na 25, waliowaona kituoni Mitengo wakihusika na suala la kumshughulikia marehemu.
“Utetezi wao kuwa hawakupokea fedha za kigeni za marehemu unapingwa na ushahidi wa shahidi wa 3, uliothibitishwa pia na shahidi wa nne wa utetezi (mshtakiwa wa nne) aliyeeleza kuwa mali zilizokamatwa, zikiwamo fedha za kigeni, zilikabidhiwa kwa mshtakiwa wa kwanza mbele ya mshtakiwa wa pili,”alisema Jaji Mwanga.
Jaji alisema mfululizo wa matukio kama yalivyoelezwa na mashahidi wa upande wa mashitaka unaelekeza moja kwa moja kwa washtakiwa hao wawili ambao ni Kalanje na Onyango kuwa ndio wahusika wa mauaji hayo.
“Kwa kiasi kikubwa, washtakiwa hawa walitoa uongo kwa kudai kuwa hawakuwahi kukutana na marehemu (Mussa) katika Kituo cha Polisi Mtwara,”alisema Jaji.
“Hata hivyo, mshtakiwa wa kwanza alikiri kufahamu na kuamuru kukamatwa kwake, na mshtakiwa wa pili alikiri kuamuru aachiwe kwa dhamana.
“Wote walikubali kuwa ingawa alikamatwa, hakuna malalamiko yaliyowahi kufunguliwa dhidi yake, na hakuna jalada la kesi lililofunguliwa dhidi yake kuhusu wizi wa pikipiki. Hivyo ni dhahiri, hawakuwa wakisema ukweli.
“Kulingana na sheria, uongo wa mshtakiwa unaweza kuunga mkono kesi ya upande wa mashitaka,”alisema Jaji Mwanga na kurejea ya Nyamhanga Joseph @ Chalicha dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 359 ya 2021.
“Ingawa mshtakiwa wa pili alikuwa tu karibu na marehemu (Mussa) alipodungwa sindano na kukabwa, tabia yake haimtakasi hata kidogo. Nia yake ya pamoja inaweza pia kuonekana kupitia kimya chake,”alisisitiza Jaji.
“Katika tukio lililofanana na hili, Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki (EACA) katika kesi ya Ongodia dhidi ya Uganda (1967) ilibainisha kuwa:
“Ingawa Erima hakuzungumza, kutikisa kichwa kwake wakati wa mkutano kulikuwa ni ishara ya kuonyesha nia ya pamoja,”alisema na kuongeza kuwa kwa uamuzi huo, hata tendo moja tu linaweza kutosha kuonesha kuwepo kwa nia ya pamoja.
“Mshtakiwa wa pili alishiriki mwanzoni mwa uchunguzi wa tuhuma alizohusishwa Mussa. Aliambatana na mshtakiwa wa kwanza hadi Kituo cha Polisi Mitengo. Alishuhudia Mussa akikabwa hadi kufa bila kuchukua hatua yoyote.
“Aliambatana na mshtakiwa wa kwanza pamoja na Inspekta Msaidizi Mahembe kuupeleka mwili wa marehemu Msitu wa Hiari. Matendo yote haya ni vitendo vya wazi vinavyotosha kuonesha nia ya pamoja,”alisisitiza Jaji Mwanga.
Alisema chini ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, marejeo ya 2019, msaidizi au mshirika wa uhalifu huchukuliwa kama mhalifu halisi au wa msingi na hushiriki kiwango sawa cha hatia na mtendaji mkuu wa kosa hilo.
“Uwepo wa mshtakiwa wa pili eneo la tukio kwa mazingira yaliyoashiria kuwa hakujitenga na kitendo kilichofanyika, unatosha kutoa hitimisho kuwa hakuwa mtazamaji tu wa tukio bali alikuwa msaidizi na mshirika wa uhalifu kwa mujibu wa kifungu cha 22(c) cha Kanuni ya Adhabu.”
Jaji Mwanga alisema baada ya kubaini hivyo, anajikuta analazimika kuhitimisha kuwa kipengele cha pili kinajibiwa kwa mtazamo chanya kuhusu mshtakiwa wa kwanza na wa pili kuwa wao ndio waliohusika na mauaji hayo.
Usikose kesho hitimisho la kiini cha tatu…