Dar es Salaam. Ingawa usafiri wa teksi mtandao unaonekana kuwa mkombozi kwa wengi kutokana na urahisi wa kupatikana kwake hususan maeneo ya mijini, kwa upande mwingine yapo mazingira yanayoweka hatarini usalama wa abiria.
Hatari ya usalama huo, inatokana na mienendo ya baadhi ya madereva kutumia akaunti zisizo zao kutoa huduma hiyo, hivyo kushindwa kupatikana iwapo watasababisha hali yoyote inayohatarisha ama maisha au usalama wa abiria.
Upo ushahidi wa waliowahi kuathiriwa na mazingira hayo na hatimaye wakashindwa kumpata dereva husika kwa kuwa akaunti haikuwa yake, kama inavyosimuliwa na Jesca Mrema, mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam.
“Nilipoomba teksi kupitia programu tumizi, picha ya dereva ilikuwa ya mwanamke lakini aliyefika kunichukua alikuwa mwanaume na nilipouliza alidai ni shemeji yake. Nilibaki kimya na kuendelea na safari kwa sababu nilikuwa na haraka,” anasema Jesca.
Isingekuwa rahisi kwa Jesca kuhoji zaidi kwa kile anachoeleza, imezoeleka kukutana na hali hiyo, ukizingatia hakujawahi kutokea madhara.
Patrick Samson, mkazi wa Tabata anasema tabia hiyo haina afya kwa jamii inayotumia mfumo huo kwa sababu wapo watu wanaowaitia wengine ikitokea tukio lolote si salama kwa upande wao.
“Unajua asilimia kubwa tunaamini teksi mtandao ni salama tofauti na zile tunazokutana nazo kwenye vituo aidha vya mabasi au nje ya hoteli, sasa kama kumekuwa na udanganyifu wa namna hii tunaanza kufikiria njia nyingine,” anasema Samson.
Kwa mtazamo wa Samson, kunahitajika umakini katika matumizi ya teksi mtandao, kwa kuwa kuna uwezekano kukafanywa vitendo vya kihalifu na muhusika asijulikane.
Kesi zaidi ya 20 zaripotiwa
Mkurugenzi Udhibiti, Usafiri wa Barabara, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano anasema mamlaka hiyo imekutana na zaidi ya kesi 20 za aina hiyo.
“Sheria na kanuni zetu zipo wazi na kampuni za teksi mtandao zinapoomba leseni zinajua kabisa ni kosa kutoa kibali kwa dereva ambaye hana leseni aliyotolewa na Latra kibiashara,” amesema.
Ili kukomesha tabia hiyo, amesema wamekuwa wakizitoza faini baadhi ya kampuni za taksi mtandao ambapo zipo walizozitoza Sh20 milioni huku madereva waliokamatwa wakitozwa Sh100,000 kila mmoja.
“Dereva anatumia akaunti ya mtu mwingine, hana leseni na abiria hana namna ya kujua ni nani hasa anayempeleka hili ni tishio kwa usalama wa abiria,” amesema Kahatano.
Amesema hii inaweka hatarini usalama wa abiria aliyebebwa kwa kuwa maelezo ya dereva yaliyowekwa hayaoani na dereva anayefika kumchukua abiria.
Kahatano amesema watu wanaweza kufikiria ni jambo la kawaida lakini inapotokea hatari inamgharimu dereva aliyegawa akaunti yake, pindi uchunguzi utakapofanyika kwani hawatamtambua yule aliyepewa.
Mmoja wa madereva, Michael Kisoki anakiri kuwepo kwa tabia za matumizi ya akaunti zisizo zao, akidai wanasaidiana.
“Kupeana akaunti ni kawaida na watu wengi wanafanya hivyo na ukifanyika uchunguzi watakutana na haya mambo kwani tumejijengea tabia yetu madereva ya kusaidiana bila kujali sheria inasema nini,” anasema Kisoki.
Anasema wanapeana akaunti kwa kufahamiana kwenye kijiwe na wanahakikisha kunakuwa na tahadhari ya kutofungiwa kwa kitendo hicho.
Dereva mwingine, Shaban Mokiwa anasema alishawahi kupewa akaunti ya rafiki yake, lilipotokea kosa alipigiwa simu na hatimaye akaunti ikafungwa.
Anafafanua kwa kuangalia haraka wanaona ni jambo la kawaida lisilo na madhara lakini ni tatizo kwani inapotokea uhalifu muhusika wa kwanza kushikiliwa ni mwenye akaunti.
“Siku zote tunafanya kazi kwa kuoneana huruma ya maisha lakini linapotokea jambo kubwa ambalo linaweza kumpeleka mtu jela ndipo tunakumbuka huruma huwa inaponza hususani kwenye masuala ya usafirishaji,” anasema Mokiwa.
Hata hivyo, madereva waaminifu kama Asha Shambalai wanaona hatua hiyo inawaweka kwenye hatari ya kutiliwa mashaka na kupoteza kuaminiwa na wateja.
“Tunaofanya kazi kwa uaminifu na kufuata sheria na kanuni tunachafuliwa na hawa wanaotumia akaunti za kupanga, wengine hata leseni hawana,” anasema Asha.
Asha anasema kampuni inapaswa kuimarisha utambuzi wa uso (face verification) kila siku, sio tu wakati wa usajili.
Licha ya kuwa na masharti ya wazi, kampuni za teksi mtandaoni zinakumbwa na changamoto ya ufuatiliaji wa matumizi ya akaunti.
Hii ni kwa sababu baadhi ya madereva wanaotumia akaunti za watu wengine wanaweza kufanya kazi kwa miezi au hata miaka bila kugundulika, hasa kama wanaendesha kwa uangalifu na wanatunza viwango vya nyota (rating).
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya teksi mtandao ambaye hakutaka jina lake liandikwe anasema wamekuwa wakiwafungia madereva wanaokiuka masharti ya usajili.
“Tukikutana na kesi ya akaunti kwa mtu mwingine na si muhusika tunachofanya ni kumuita ofisini na kumueleza makosa yake kisha tunamfungia na hii tumefanya kwa madereva kadhaa,” anasema.
Anasema wanafanya hivyo kwa sababu madereva wanaokamatwa kwa kwenda kinyume na usajili rungu linawaangukia wao kutoka kwa Serikali.
Ili kuepuka jambo hilo, anasema wamekuwa wakihamasisha abiria kutoa taarifa endapo amechukuliwa na dereva asiyefanana na picha inayotokea kwenye programu.
Changamoto hiyo, imeifanya Latra kuandaa mpango wa kutoa motisha kwa abiria watakaotoa taarifa za madereva wasiowiana na taarifa za akaunti.
“Tumeandaa mpango huu ili kupata taarifa kwa haraka kupitia wananchi kuhusu udanganyifu unaofanywa na madereva kwa sababu mamlaka hiyo haina watu wa kutosha kufuatilia kila sehemu,” amesema.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Kahatano anawashauri abiria kuhakikisha taarifa za dereva aliyefika zinawiana na zile zilizo kwenye mfumo wa program.
Aidha, anawatahadharisha abiria kutokubali kukatisha safari wanaposhawishiwa na madereva wa bodaboda au teksi mtandao kwani hatua hiyo inawaondolea kinga ya kiusalama.