HOMA ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) imezidi kupanda, huku zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kufungwa kwa zoezi la uchukuaji na urudishwaji wa fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya shirikisho hilo.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 16 mwaka huu jijini Mwanza na nafasi zinazowaniwa ni Rais wa RT (nafasi moja), Makamu wa Rais (nafasi moja), Mjumbe wa viti maalum wanawake (nafasi moja) na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji (nafasi nne).
Miongoni mwa wanaowania nafasi ya juu ya urais ni Rogath John Stephen Akhwari, mtoto wa gwiji wa zamani wa riadha wa Tanzania, John Stephen Akhwari na amejitosa kuwania nafasi hiyo akimkabili Silas Isangi anayetetea kiti chake.
Ushindani wa urais kati ya Rogath na Isangi unaonekana kuwa kivutio kikubwa, hasa ikizingatiwa historia ya familia ya Akhwari katika riadha na nafasi ya Isangi kama kiongozi aliyepo madarakani.
Rogath ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA) na Kocha wa timu ya riadha ya Jeshi la Polisi Tanzania, amethibitisha rasmi kuchukua na kurejesha fomu ya kuwania urais wa RT.
“Ni kweli nimechukua fomu ya kuwania urais wa RT na tayari nimeirejesha kwa sababu ilikuwa inatolewa kwa njia ya mtandao na kurudishwa kwa njia hiyo.
“Hakuna kingine naweza kuongea kwa sasa ila naamini kila kitu kitakwenda sawa kwa sababu maisha yangu yote nimeishi katika mchezo huu wa riadha,” alisema Rogath.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya RT, Leonard Thadeo, baada ya kufungwa kwa zoezi la kuchukua na kurudisha fomu Julai 18, hatua itakayofuata ni usaili wa wagombea wote Julai 25.
Agosti Mosi, majina ya waliopitishwa yatatangazwa, kisha Agosti 2 hadi 8 kupokelewa, kusikilizwa na kutolewa kwa uamuzi wa mapingamizi, kisha Agosti 9 hadi 16 ni kipindi rasmi cha kampeni na Agosti 16 Uchaguzi mkuu kufanyika Mwanza.