Upelelezi kesi ya wanachuo wanaodaiwa kumjeruhi mwenzao, wakamilika

Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya kusababisha madhara mwilini inayomkabili mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mary Matogolo (22) na wenzake wawili, umekamilika.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Julai 14, 2025 wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Mary na wanafunzi wenzake wanakabiliwa na mashtaka manane, likiwamo la kutishia kuua, kutoa taarifa za uwongo mitandaoni na uharibifu wa mali za mwanafunzi mwenzao.

Mbali na Mary wanafunzi wengine katika kesi hiyo ni Ryner Mkwawili wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam (ARU) na Asha Juma, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA).

Wakili Kamala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamula, anayesikiliza kesi hiyo.

“Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake umekamilika, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali (PH) washtakiwa hawa,” amedai Wakili Kamala.

Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, 2025 kwa ajili upande wa mashtaka kuwasomea hoja za awali.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kula njama za kutenda uhalifu.

Katika shtaka hilo, kwa pamoja wanadaiwa Machi 16, 2025, eneo la Sinza Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuchapisha taarifa za uongo.

Shtaka la pili la kusabambaza taarifa za uongo linawakabili Mary na Asha, kwa kusambaza taarifa za uongo, katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno, “toa  sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi.”

Shtaka la tatu ambalo pia ni kusambaza taarifa za uongo linalomkabili, Ryner peke yake, anadaiwa siku hiyo alisambaza taarifa hizo kupitia mtandao wa WhatsApp.

Shtaka la nne ambalo ni kusababisha madhara makubwa, linamkabili Mary peke yake, akidaiwa siku hiyo alimshambulia Magnificant Kimario kwa kumpiga kichwani na chuma na hivyo kumsababishia maumivu makali.

Shtaka la tano ambalo ni kusababisha madhara makubwa, ambalo linawakabili washitakiwa wote.

Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja kwa kutumia nguvu walimvuta nywele Magnificant na kusababisha madhara makubwa.

Shtaka la sita na saba, ambayo ni kuharibu mali, pia yanamkabili Mary peke yake.

Inadaiwa Mary aliharibu laini ya simu na simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000, mali ya Magnifcant.

Shtaka la nane  ni kutishia kuua, ambalo linawakabili washtakiwa wote, wanadaiwa siku ya tukio, walimtishia kumuua. Magnificant kwa kutumia kisu.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka yao.

Related Posts