MBARONI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA MKEWE KILOSA


Farida Mangube, Morogoro
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia James Lugembe (55), mkazi wa Kitongoji cha Manzese B, Kata ya Mkwatani, Wilaya ya Kilosa, kwa tuhuma za kumuua mke wake, Restuta Walela (50), kwa kumkata kwa kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Alex Mkama, amesema tukio hilo la kusikitisha limetokea usiku wa kuamkia Julai 13, 2025.
Kamanda Mkama amesema baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa alijaribu kujiua kwa kunywa sumu, na kwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mvutano wa kifamilia, ambapo marehemu alilalamikia mumewe kwa kushindwa kutimiza majukumu ya kifamilia, huku mume akimtuhumu mkewe kwa ulevi na kuchelewa kurudi nyumbani mara kwa mara.
“Uchunguzi wa tukio hili unaendelea kwa kushirikiana na wadau wa haki jinai, na mara utakapokamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa,” amesema Kamanda Mkama.
Aidha, Kamanda huyo ametoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayekwepa mkono wa sheria.
Jeshi la Polisi limeendelea kuhimiza jamii kutatua migogoro ya kifamilia kwa njia ya mazungumzo na kuomba msaada wa kitaalamu ili kuepusha matukio ya kikatili kama hilo.

Related Posts