Wasira: Amani ienziwe, si hewa ipatikanayo bila kulipiwa

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema suala la amani ya Tanzania lisichukuliwe kama hewa inayopatikana bila kulipiwa chochote, bali ni mipango na uzalendo wa viongozi ambao unapaswa kuendelezwa.

Amehimiza Watanzania wakiongozwa na viongozi wa dini kuendelea kudumisha misingi iliyosimamisha amani iliyowekwa na waasisi wa Taifa.

Wasira ameyasema hayo leo Julai 14, 2025 wilayani Maswa mkoani Simiyu alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Nyalikungu.

“Historia ya Afrika imetupa amani kwa miaka mingi, lakini watu wengine wanafikiri hii amani ipo tu kama hewa, maana hewa hatulipii. Nataka niwaambie amani hii ina mkono wa mtu.

“Historia ya nchi yetu ina waasisi ambao walifanya mambo ambayo Afrika hawakuwahi kuyafanya. Waliunganisha watu wa makabila yote tukawa kabila moja linaitwa Tanzania, waliunganisha watu wote wa dini zote tukawa kitu kimoja, haya mambo sio rahisi sana kama tunavyofikiri na haiwezekani Mwenyezi Mungu akaumba nchi moja tu akaipa amani, lakini Mungu anatumia wanadamu katika kutenda kazi yake,” amesema Wasira.

Hivyo, amewataka kutambua kuwa Mungu alitumia waasisi kuifanya Tanzania jinsi ilivyo sasa na kazi iliyo mbele ya Watanzania kwa sasa ni kuiendeleza kwa kuilinda na kuidumisha.


Amesema, “haiwezekani ukienda kaskazini kuna matatizo, ukienda kusini kuna matatizo, ukienda magharibi kuna matatizo, lakini hapa katikati nchi inaitwa Tanzania tunaishi kwa amani bila ubaguzi wa makabila wala wa dini, ndio maana mimi mgeni rasmi lakini dini yangu hamuijui,” amesema.

Kupitia hafla hiyo, Wasira amewasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan aliyesema anatambua mchango wa viongozi wa dini katika kuimarisha umoja na amani ya nchi.

“Sasa nawapa salamu za Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, Rais Samia na kwa sababu nilimwambia nimealikwa mahali hapa kuwa mgeni rasmi kwa ajili ya mchango wa kanisa na yeye ni mchaMungu, akaniambia na yeye atachangia Sh50 milioni ,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amewasihi Watanzania kuendelea kumuombea Rais  Samia aendelee kuongoza taifa lenye uvumilivu la watu wanaovumiliana, kupendana, wenye furaha na ustawi.

Pia, amewaomba viongozi wa kanisa kuendelea kuiombea nchi hususan katika mwaka huu wa uchaguzi mkuu ili ufanyike kwa uhuru, amani na haki.

“Naamini kabisa kwamba mnafahamu mwaka huu ni wa uchaguzi, tunaliomba kanisa, tunawaomba viongozi wetu wa kanisa, tunawaomba waumini wote tuliombee Taifa letu tunapopita katika uchaguzi huu uwe wa amani ulio huru lakini zaidi utakaotupatia viongozi watakaoendelea kuliongoza Taifa hili,” amesema.

Akitoa salamu za shukurani, Paroko wa Parokia hiyo, Padri Deogratius Ntindiko, amemshukuru Rais Samia kwa kuguswa na ujenzi huo na kuchangia kiasi hicho cha fedha.

“Kupitia nafasi yako (Wasira), tunamshukuru sana Rais Samia, amegusa nyoyo zetu, amegusa matarajio yetu kwa mchango wake wa Sh50 milioni  sisi wana Nyalukungu tunamuombea,” amesema paroko huyo.

Related Posts