Lindi. Abdallah Mwenda (70) mkazi wa Mchinga Manispaa ya Lindi amekutwa amefariki kando ya fukwe ya Bahari ya Hindi baada ya kutorudi nyumbani kwao tangu Julai 13,2025 alipokwenda kuvua samaki.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Jumatatu Julai 14,2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori imeeleza kuwa Mwenda alikwenda kuvua samaki kwa kutumia mtumbwi wake Julai 13,2025 asubuhi na hakurudi nyumbani kwao hadi Julai 13 walipoukuta mwili wake pembezoni mwa Bahari ya Hindi saa 12 jioni.
Taarifa ya Imori imeeleza kuwa Mwenda alikuwa anafanya uvuvi kwa kutumia ndoano na mwili wake haukuwa na majeraha yoyote.
“Mwili wa marehemu ulikutwa kwenye fukwe ya Bahari ya Hindi ambapo ulionesha kutokuwa na majeraha yoyote.”amesema Imori
Imori amewataka wavuvi na wakaazi wa maeneo ya fukwe kuchukua tahadhari katika shughuli zao za uvuvi hasa kwa wazee na wanaovua peke yao.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Mchinga kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitabibu, ili kubaini chanzo halisi cha kifo.
Mvuvi Chedu Chedu amemuelezea marehemu Mwenda kuwa alikuwa ni mzee mwenye busara na upendo kwa watu wote.
“Tumepata pigo sana kwa kuondokewa na mzee wetu kwani alikuwa anapenda utani, mcheshi na mwenye busara, kifo chake kimetuumiza sana sisi wavuvi wa Mchinga,”amesema Chedu.