Hersi ataja mambo matatu usajili mpya Yanga

RAIS wa Yanga, Hersi Said amesema wana mambo matatu magumu kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa ambayo wanatakiwa kuyazingatia ili kufikia mafanikio msimu ujao.

Hersi amefunguka hayo alipozungumza na Mwanaspoti ambapo amesema jambo la kwanza ni kusajili nyota wenye uzoefu mkubwa, pili kuwa na benchi la ufundi bora ambalo litaendana na ubora wa wachezaji waliopo na tatu kubakiza nyota wanaohitajika zaidi kikosini.

“Unajua tuna malengo ya kufanya vizuri kimataifa lakini pia tuna deni kubwa la kuhakikisha tunabakiza mataji yote tuliyotwaa msimu uliopita, hili kwetu linatupasua kichwa, bila uwekezaji hatuwezi kufanikiwa,” alisema na kuongeza.

“Ukiondoa wachezaji waliopo ambao wamefanya makubwa baadhi kwa misimu minne yote mfululizo na wengine wapya, tumekuwa hatupo bora kimataifa kama matarajio yetu, hivyo dirisha hili mpango wetu ni kusajiili wachezaji bora zaidi na wenye uzoefu ili tuweze kufikia malengo.”

Hersi alisema wanachokifanya dirisha hili anakiri kuwa ni kitu bora zaidi na hakijawahi kutokea ndani ya misimu minne iliyopita kwenye sekta ya usajili wakizingatia ubora na mahitaji muhimu yaliyopo ili kulipa madeni ndani na kuwa na muendelezo mzuri kimataifa.

“Kimataifa hatuna muendelezo mzuri na asikwambie mtu kwenye michuano hiyo uzoefu unahitajika sana na sisi kila msimu tumekuwa tukipunguza wachezaji kwa kuuza au wengine kuamua kutafuta changamoto nyingine, hivyo tunakuwa na maingizo mapya,” alisema na kuongeza.

“Kutokana na hayo, msimu huu tunapambana kubaki na nyota wote muhimu ambao wana mikataba na waliomaliza lakini pia naahidi kuwa usajili unaofanywa sasa mashabiki na wanachama watanielewa tukianza kuwatambulisha ila nafikiri  utakuwa usajili bora kuliko sajili ambazo tumewahi kuzifanya miaka ya hivi karibuni.”

Alisema pamoja na kubeba mataji yote ya ndani msimu uliomalizika, lakini bado wana deni kubwa kwa wana Yanga kubeba tena mataji yote  na kufanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa na ili wafanye hivyo wanahitaji uwekezaji.

Msimu wa 2024-2025, Yanga ilitetea mataji mawili ambayo ni Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, pia ikaweka nyongeza kwa kubeba Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano ambayo yote yalikuwa mikononi mwa Simba. Pia ikashinda Kombe la Toyota, michuano iliyofanyika Afrika Kusini wakati wa maandalizi ya msimu.

Katika usajili, inaelezwa tayari Yanga imemalizana na mshambuliaji Celestine Ecua raia wa Ivory Coast ambaye msimu wa 2024-2025 amekuwa Mchezaji Bora (MVP) wa Ligi Kuu ya Ivory Coast akifunga mabao 15 na asisti 12.

Related Posts