Dar es Salaam. Wadau wa siasa na diplomasia wamepokea kwa mtazamo tofauti uamuzi wa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole wa kujiuzulu katika nafasi hiyo huku wakiuhusisha na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Baadhi ya wadau hao wameeleza kwamba ni haki yake kujiuzulu kulingana na sababu alizonazo, hata hivyo wamebainisha kwamba njia aliyoitumia kuweka mitandaoni barua aliyoituma kwa Mamlaka yake ya uteuzi, Rais, siyo sahihi.
Katika barua yake, aliyomwandikia Rais Samia Suluhu Hassan, jana Julai 13, 2025, Polepole ameeleza kusikitishwa na kile alichokiita mwelekeo wa uongozi usiojielekeza katika kusimamia haki, amani na kuheshimu watu.
Polepole ameeleza kwamba kwa muda ambao amekuwa akitumikia Taifa ndani na nje ya nchi, ameona na kushuhudia mambo ambayo yamemfanya akose amani ndani ya moyo wake, hivyo ameamua kukaa pembeni.
Wakizungumzia uamuzi wa Polepole, wachambuzi wa siasa na diplomasia wamebainisha kwamba Balozi Polepole ana haki ya kujiuzulu, lakini kuweka barua yake mitandaoni hakuwa sahihi kwa kuwa siyo utaratibu wa utumishi wa umma.
Mwenyekiti wa Mabalozi wastaafu nchini, Dk James Nsekela amesema utaratibu wa kawaida wa mfanyakazi kujiuzulu ni kuandika barua kwa mwajiri au mamlaka ya uteuzi, lakini kwa sababu Polepole ni mwanasiasa, huenda ana sababu zake.
“Kwa utaratibu wa kawaida, ni kama unavyoomba kazi kwa mwajiri, ukijiuzulu unamwandikia barua huyo huyo. Na kwa kawaida, unampa privilege (nafasi ya kipekee) yule aliyekuteua ya kusema atakachokisema wakati anajaza nafasi yako.
“Tuseme tu kwamba tuko kwenye kipindi cha uchaguzi, kwa hiyo tusichemke sana, tuone tu kwamba mtu amefanya alichokifanya kwa madhumuni yake na hatuwezi kujua madhumuni ya mtu mbali ya hicho tunachokisoma,” amesema.
Dk Nsekela amebainisha kwamba siyo mara ya kwanza kwa Balozi kujiuzulu, anakumbuka iliwahi kutokea mwanzoni mwa miaka ya 1960 ambapo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Kasanga Tumbo aliamua kujiuzulu.
“Siwezi kukumbuka mara moja sababu alizozitoa, lakini nadhani…unajua kazi ya ubalozi inakufanya uwe mbali na nchi yako, kwa hiyo inawezekana ni kama alivyoeleza Polepole kwenye barua yake, kwamba anatamani kuwepo nchini, na yule wakati ule sababu zilikuwa ni hizohizo,” amesema.
Amefafanua kuwa kuna mabalozi wanasiasa na mabalozi kitaaluma (career diplomats) ambao wanakuwa ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje. Amesema mabalozi wa kitaaluma wakijiuzulu linakuwa jambo la ajabu kwa sababu itakuwa ni kuacha kazi moja kwa moja tofauti na wa kisiasa ambao anakuwa ameteuliwa kwa kipindi fulani.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Denis Konga amesema balozi anapokuwa nje ya nchi, mbali na kuwakilisha nchi, anamwakilisha Rais, hivyo kujiuzulu ni utashi binafsi wa kukataa hayo majukumu.
Kisiasa, amesema kuna mambo mengi na kwenye barua yake amezungumzia utaratibu, demokrasia, haki na wajibu. Amesema barua hiyo inaonyesha kwamba ana msigano na wengine, hawaendani na ameamua kuondoka.
Kidiplomasia, amesema ipo kwa maana ya haki alizozizungumzia ikiwemo ya kutoshiriki na wengine bila kuharibu utaratibu uliowekwa
“Jambo muhimu ni; je, chama kinachounda Serikali na kiongozi mkuu wa nchi anatoka kwenye chama hicho, wao wanamuonaje? Wakati mwingine tunahisi labda kuna mnyukano mkubwa ndani ya chama.
“Hoja hii imekuwa baada ya majina kuanza kukatwa kwenye wilaya na mikoa, sasa tunasubiri uamuzi wa kamati kuu ya watu 23 ambao wao watakuja kutoa majina rasmi ya kwenda kupigiwa kura na wajumbe. Kwa hiyo hatujui nini kipo huko ndani,” amesema Konga.
Kwa upande wake, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amesema mkataba wowote wa kazi yeyote anaweza akauvunja wakati wowote, mwajiri au mwajiriwa, mamlaka ya uteuzi au mteuliwa.
“Ni haki yake kuamua kama alivyoamua, hatuwezi kuihoji. Amejipima mwenyewe. Mimi binafsi kama balozi, kazi ya ubalozi ni ya heshima kubwa sana angeweza kuandika barua kama hiyo.
“Hii ya kupita kwenye mitandao si utaratibu serikalini, hilo ndilo linaleta ukakasi. Angeweza barua asiiweke kwenye mitandao, ikishafikia mamlaka akasubiri ajibiwe, halafu baadaye akaja kutoa habari kwa umma,” amesema.
Dk Bana ameongeza kwamba; “Kwa mtu ambaye ni balozi na ameshika nafasi za juu katika utumishi wa umma, kwa kweli huo mwenendo haukubaliki kwa maana ya maadili. Lakini hili la kuachia ubalozi ni haki yake.”
Balozi huyo amesema ukidadisi uamuzi huo wa Polepole kwa mapana na marefu, unapata maswali; kwa nini atoe barua wakati huu ambao Taifa limeingia kwenye mchakato wa uchaguzi, jambo ambalo linavuta hisia za watu wengi.
“Kwa hiyo, timing yake ndiyo inaibua maswali, muda aliofanya uamuzi huo unaweza kuwafanya watu waibue maswali mengi na wahusishe na uchaguzi. Lakini kwa kuwa yeye mwenyewe hajasema…tusubiri, hakuna kinachofichika,” amesema.
Mchambuzi wa siasa, Buberwa Kaiza amesema Polepole katika barua yake, ameeleza mambo mengi ambayo tafsiri yake ni kwamba boti ya utawala haiendi sawa, watu wanatekwa, wengine wanauawa lakini Serikali haisemi chochote.
“Kwa kuwa alikuwa hajisikii vizuri kuwa ndani ya Serikali, Polepole amesema amelazimika kufanya hivyo (kujiuzulu) ili asiwe kundi moja na watu ambao hawalitakii mema Taifa hili na wale anaoona hawafai,”amedai Kaiza.
“Muda wa uchaguzi na mabadiliko, hoja za watu juu ya utendaji wa Serikali, masuala ya Katiba na haki za binadamu, utawala bora na mambo mengine, vimekuwa ni sababu mojawapo ambayo imechangia uamuzi wake kuondoka serikalini,” amesema Kaiza.