Mchezo mchafu watiania CCM wafichuliwa

Dar/mikoani. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeanza vikao vya mchujo wa majina ya wagombea ngazi ya kitaifa, huku kikisema kimebaini michezo michafu inayofanywa na watiania, ikiwamo kuziingilia kamati za siasa na kuchafuana.

Pia, kimeeleza utaratibu wake wa kupendekeza watiania, unahusisha alama A hadi E na anayepewa ya kwanza ndiye anayestahili zaidi na ya mwisho hastahili kupendekezwa, huku wenye historia ya uongozi hupewa B.

CCM inaeleza hayo, katikati ya madai kuwa, wapo wanasiasa waandamizi waliotemwa mapema katika michujo ya awali ya watiania, huku Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mikoani, ikikiri kuwepo viashirikia, malalamiko na tuhuma za vitendo hivyo kwa watiania hao.


Hayo yote yanakuja wakati ambao, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi, ameanza kukutana na wajumbe wa sekretarieti ya Halmashauri Kuu Taifa, tayari kuanza uchambuzi wa majina ya watiania.

Kikao hicho, kinachotarajiwa kuendelea hadi Julai 16, 2025 kimeitishwa kufuatia kukamilika kwa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uteuzi wa nafasi za uwakilishi.

Nafasi hizo zinahusisha ubunge wa majimbo, ujumbe wa baraza la wawakilishi, viti maalumu vya ubunge na baraza la wawakilishi pamoja na udiwani.

Shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu kwa chama hicho, ilifunguliwa kuanzia Juni 28 hadi Julai 2, 2025. Vikao vya kamati za siasa za wilaya na mikoa navyo vimekwishamaliza kupendekeza majina ya wagombea.

Julai 19, 2025, kunatarajia kufanyika kikao cha kamati kuu cha uteuzi wa majina yasiyozidi matatu ya wagombea ubunge na uwakilishi katika kila jimbo.

Baadhi ya maeneo imesikika minong’ono kwamba, wamekatwa majina ya watiania wenye majina makubwa wakiwamo wabunge wanaotetea na wabunge wa zamani waliowahi kuwa mawaziri.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla akizungumza jana Jumapili, Julai 13, 2025 juu ya kinachoendelea, amesema hadi sasa hakuna mgombea yeyote aliyekatwa au kuenguliwa, kwa kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu majina ya wagombea utatolewa na Kamati Kuu ya CCM.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia taarifa zilizozagaa mitandaoni zikidai kwamba, kuna wagombea waliokatwa katika ngazi ya mikoa na wilaya.

Amesema mchakato wa awali wa ukusanyaji maoni kuhusu watiania umekamilika katika ngazi za kata, kamati za siasa za wilaya na za mikoa.

“Kwa utaratibu na mchakato ndani ya chama, hakuna mtu aliyeenguliwa au kukatwa. Nimeona (mitandaoni) watu wakiandika fulani kafyekwa, hayumo kwenye tatu bora. Naomba mtupelekee ujumbe; hakuna aliyeenguliwa, hakuna aliyekatwa, hakuna aliyefyekwa. Huo ni mchakato unaoendelea ndani ya chama chetu,” amesema.

Michezo michafu hiyo iliyobainika, imewekwa wazi leo, Jumatatu, Julai 14, 2025 na Katibu wa Kamati Maalumu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto alipozungumza na Mwananchi.

“Tumebaini kuna changamoto wapo waliochafuliwa, wapo walitengenezewa sifa za maadili feki ili kumharibia aonekane hafai,” amesema.

Mbeto amesema wapo waliowarubuni baadhi ya makada wasio na sifa wakagombee nao kama vivuli, ili kurahisisha mazingira ya kupendekezwa.


“Mtu anamshawishi mwanamke akachukue fomu, anamlipia fedha, anamshawishi mtu asiye na sifa ili kutengeneza watu vivuli, anajua akiingia nao kwenye ushindani lazima yeye ndiye atakayependekezwa,” amesema.

Amesema wanafanya hivyo, ili kupunguza ushindani, hivyo kunakuwa na wagombea kadhaa ambao kiuhalisia wanasimama kama vivuli vya wengine.

“Ndio maana tukawa tunasema vikao hivi vitende haki maana wao wanaweza kufanya leo, lakini uamuzi wake una athari kubwa kwa miaka mitano unampeleka kiongozi bubu bungeni, barazani anakwenda kulala tu hachangii anamaliza Bunge hajawahi kusimama hata mara moja,” amesema.

Dhamira ya chama hicho, amesema ni kupata wagombea wenye sifa ili kuwashindanisha.

“Watu wenye sifa uwezo, kukaa kwenye chama na kujenga hoja lakini kilichotokea ni kinyume chake watu wamepanga watu wao makusudi na kutengenezewa ajali,” amesema.

Kwa kuwa chama hicho kina vyombo makini ikiwamo kamati za maadili, amesema anaamini zitashauri vema ili kamati kuu itende haki na kupitisha watu kulingana na uwezo na heshima zao.

Hata hivyo, Mbeto amesema tayari kuna uamuzi uliochukuliwa, ingawa hakuutaja, amesisitiza vikao vya uteuzi baada ya kukusanya maoni na kuangalia ushahidi na kujiridhisha kama havikuingiliwa ndivyo vitakavyotoa hatima.

Katika mchujo wa wagombea, Mbeto amesema ngazi za chini wanatumia alama A, B, C, D na E, kila moja ina maana yake na imebainika baadhi ya watiania wamepewa wasizozistahili.

Kiongozi huyo amesema alama A wanapewa marais, B inamaanisha anafaa kuwa kiongozi au alishakuwa kisiasa au kiserikali, C anafaa na ajaribiwe, D mwenye upungufu wa maadili na E hafai kupendekezwa.

Amesema kwa watu waliowahi kuwa viongozi, wanapopewa alama D au E lazima, yaambatanishwe maelezo ya kwanini imekuwa hivyo.

“Ukimpa nafasi ndogo lazima uambatanishe na maelezo ya kujitosheleza kwanini, ilhali alikuwa tayari ni kiongozi, huu ndio utaratatibu wa CCM,” amesema.

Katika mchakato huo, Mbeto amesema wamebaini viongozi wengi wenye fedha au waliokuwa wanashikilia majimbo, wamecheza michezo michafu ili kutengeneza mazingira ya wale wanaoonekana tishio kwao waondolewe.

“Ili upendekezwe chama kinaangalia umepewa alama gani, sio rahisi kwenye chama chetu kwamba mtu hajapewa alama kuanzia ngazi ya chini halafu huku juu ukapewa sasa kama haya yajazingatiwa ndio maana unakuta haki haitendeki,” amesema.

Amesema kulifanyika semina kwa wajumbe wa kamati za siasa za wilaya, majimbo na mikoa kujua maana ya alama wanazopaswa kupewa wagombea, ili kuepusha usumbufu na kumwonea yeyote.

Wakati hali ikiwa hivyo, Kamanda wa Takukuru Shinyanga, Donasian Kessy amekiri kusikia tetesi za watu kujihusisha na vitendo vya rushwa na kwamba wanafuatilia kupata uhakika.

“Na sisi tunasikia tetesi tumeanza kufuatilia, hakuna taarifa yoyote tuliyoipata na ushahidi wake, kwa hiyo hatuwezi kusema kuna uthibitisho wenye mashiko ni tetesi tu,” amesema.

Kwa upande wa kamanda wa taasisi hiyo mkoani Mara, Mohamed Shariff amekiri kupokea malalamiko na tuhuma za vitendo hivyo katika mchakato huo, ingawa hakuweka wazi idadi kamili.

Hata hivyo, amesema tayari wameanza uchunguzi na watakapokamilisha, watuhumiwa watatiwa hatiani na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Amesema ushahidi ndiyo changamoto inayowakabili katika kushughulikia vitendo hivyo, akisema taarifa zinazowasilishwa wanakosekana mashahidi wa kutoa maelezo.

“Kuna mtu analeta taarifa kuwa fulani kaombwa au kaomba rushwa sasa ukimtaka akupe maelezo kwa kina anakataa au huyo anayedai kuombwa rushwa ukimuita ili aje akupe taarifa vizuri anakataa, kwa hiyo hii inasababisha changamoto kubwa na kutulazimu kuachana na lalamiko hilo,” amesema.

Katika Mkoa wa Arusha, Kamanda wa Takukuru mkoani humo, Zawadi Ngailo amesema kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia kama kuna watu wanaowahoji au kufuatilia tuhuma zozote za rushwa.

“Ni wazi kweli kunapokuwa na uchaguzi kuanzia ngazi za awali tunakuwa makini na kufuatilia mchakato wote,” amesema.

Takukuru mkoani Mbeya imeeleza kuwa,  inaendelea na uchunguzi kuhusu malalamiko iliyopokea kutoka vyama vya siasa kwa wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.

Takukuru imeeleza kuwa, inaendelea na uchunguzi wa tuhuma za rushwa sio kwa makada wa CCM pekee, bali vyama vyote vya siasa vitakavyobainika kuhusika.

Mkuu wa taasisi hiyo mkoani humo, Maghela Ndimbo amesema hadi sasa inaendelea na uchunguzi kwa kujiridhisha na ushahidi kutokana na malalamiko iliyopokea kutoka kwa wanasiasa.

Amesema baada ya kukamilisha uchunguzi, taarifa zitawasilishwa kwa mkuu wa Takukuru nchini au vyama husika kwa hatua zaidi, akisisitiza kuwa chombo hicho kinahitaji usawa katika kipindi hiki.

“Bado tunaendelea na uchunguzi kwa ambao tuliwahoji, lakini ieleweke kwamba, hatuangalii CCM pekee bali vyama vyote,  kwa kuwa malalamiko yapo na sisi tunaendelea kushughulika nayo,”amesema Ndimbo.

Hatua kama hizo zinafanywa pia na Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Mussa Chaulo akisema wamepokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa watiania wa ubunge CCM, lakini bado ushahidi haukupatikana.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Kristian Nyekize amesema wamepokea taarifa za tuhuma za rushwa, wanafuatilia kwa karibu ili kubaini na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

“Tunafuatilia kwa karibu michakato yote inayoendelea na tumeshapokea taarifa kadhaa za tuhuma za watiania kutoa rushwa ambazo tunazifanyia kazi, pale ushahidi utakapokamilika tukajiridhisha wahusika wote tutawachukulia hatua za kisheria,” amesema Nyekize.

Amesisitiza taasisi hiyo itawafikisha mahakamani na kuwafungulia mashtaka watakaothibitika kutoa rushwa katika hatua yoyote ya mchakato wa uchaguzi.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Holle Makungu amesema kumekuwa na malalamiko ya viashiria vya rushwa na wameshaweka mikakati kuwanasa watakaohusika.

“Siwezi kusema hakuna rushwa kabisa, lakini hatua ya awali ya mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu na vikao vya mchujo watiania CCM ngazi ya wilaya na mkoa kwa hapa Temeke imemalizika vizuri licha ya malalamiko kadhaa ambayo tumeyashughulikia ndani ya Takukuru mkoa,” amesema Makungu.

Amesema wanafuatilia na kusubiri hatua inayofuata ya majina matatu ili kuona wagombea gani watakaojihusisha na rushwa ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Hali ya rushwa inaonekana kupungua licha ya viashiria kadhaa kuripotiwa na kushughulikiwa ndani ya mamlaka yetu, hii inaonesha umma unaongeza uelewa juu ya madhara ya rushwa,  hivyo kuwa na ushirikiano chanya na mamlaka katika kupambana na rushwa,” amesema Makungu.