MWALIMU AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA KWA KULAWITI MWANAFUNZI

:::::::

Na Mwandishi Wetu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita, imemuhukumu kifungo cha maisha mwalimu wa shule ya msingi Waja Springs, Josephat Masenema kwa kosa la kumuingilia kinyume cha maumbile mwanafunzi wa darasa la tatu shuleni hapo.

Kitendo hicho alifanyiwa mwanafunzi mwenye umri wa miaka saba (7) na kwa mujibu wa hukumu iliyosomwa mahakamani hapo Juni 3 na Juni 18, mwaka huu, ni kinyume cha sheria, kifungu cha 154 (1) (a) na (2) cha kanuni ya Adhabu, sura ya 16.

Mwalimu Masenema alifunguliwa kesi ya Jinai Na. 32126/2024 baada ya kudaiwa kutenda kosa hilo Septemba 27, 2024 shuleni Waja Springs, Mtaa wa Bombambili, mkoani Geita

Keshi hiyo imesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, C.Waane, ambapo upande wa mashitaka ulileta mashahidi kadhaa wakiwamo; mama mzazi wa mtoto, mtoto mwenyewe, afisa usitawi wa jamii, dakitari wa hospitali ya serikali pamoja na maafisa wa polisi.

“Ushahidi uliotolewa mahakama imejilidhisha bila shaka kuwa umetosha kumtia hatiani mshitakiwa, mtoto ameeleza kwa uaminifu mbele ya mahakama kuwa mwalimu wake, Josephat Masenema alimuingilia kinyume cha maumbile akiwa katika choo cha shule,” Hukumu ya Hakimu Waane inaeleza.

Sambamba na ushahidi wa mtoto, fomu Na. 3 ya matibabu (PF3) inayotolewa na polisi nayo kwa mujibu wa dakitari wa serikali aliyempima, ilionyesha mtoto kuwa na dalili za majeraha yaliyotokana na kuingiliwa kinyume na maumbile.

Hata hivyo, pamoja na mshitakiwa kukana shitaka akidai siku inayodaiwa alitenda kosa ilikuwa siku ya michezo shuleni hapo, hivyo yeye (Masenema), walimu wengine pamoja na wanafunzi walikuwa uwanjani, mahakama iliutupilia mbali utetezi wake baada ya kushindwa kuuthibitisha.

Hakimu Waane akisoma hukumu hiyo Juni 3 na Juni 18 mwaka huu, alisema mshitakiwa amekutwa na hatia ya kutenda kosa la kumuingilia kinyume cha maumbile mtoto mwenye umri wa miaka nane (kwa sasa) hivyo anahukumuwa kifungo cha maisha.

Mwisho

Related Posts