Gamondi anataka majembe ya kazi Singida Black Stars

KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi anatarajia kuwasili nchini mwisho wa mwezi huu huku akiutaka uongozi wa timu hiyo kumsajilia nyota wenye uzoefu ambao watampa taji na kutoa ushindani kimataifa.

Gamondi anarudi nchini kwa mara ya pili baada ya kuinoa Yanga kwa mafanikio na kuondoka Novemba 2024 akikaa kwa takribani msimu mmoja na nusu. Sasa anarudi kuwa kocha wa Singida BS yenye tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida BS, kimeliambia Mwanaspoti kuwa Gamondi anakuja nchini mwisho wa mwezi huu na akifika wataingia kambini Agosti Mosi tayari kwa maandalizi ya msimu mpya.

“Gamondi anakuja nchini mwishoni mwa mwezi huu, akifika tu siku inayofuata timu itaingia kambini kwa ajili ya kujifua na msimu mpya ambao tunaamini utakuwa bora kulingana na sajili zilizofanywa.”

Akizungumzia mipango ya usajili mtoa taarifa huyo alisema Gamondi ameshirikishwa kwa asilimia kubwa na amependekeza kusajiliwa nyota wenye uzoefu mkubwa ili waweze kuibeba timu hiyo ndani na kimataifa.

“Gamondi ametaka nyota wazoefu ndio wachukue nafasi kubwa kwenye usajili akiamini kuwa watakuwa chachu ya wao kubeba ubingwa lakini pia kuonyesha ushindani kimataifa.”

Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta ofisa habari wa klabu hiyo, Hussein Masanza ambaye alithibitisha kuwa kambi yao wataanza Agosti Mosi mwaka huu.

Alipoulizwa kuhusu ujio wa kocha Gamondi alisema atawasili wakati wowote kuanzia sasa na wanaamini akirudi tu atapata mapumziko ya muda na kuingia kazini kujenga kikosi cha ushindani.

“Kambi tunatarajia kuanzia Agosti 1, Gamondi muda wowote kutoka sasa atawasili nchini tayari kwaajili ya kuiweka mguu sawa timu kuelekea msimu ujao ambao kwetu utakuwa wa mashindano mengi ndani na kimataifa,” alisema Masanza.

Related Posts