Baresi anukia Tanzania Prisons | Mwanaspoti

LICHA ya Amani Josiah kuiepusha Tanzania Prisons na janga la kushuka daraja msimu wa 2024-2025, inaelezwa mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, ambaye kwa sasa yupo huru.

Baresi aliyeifundisha timu hiyo kwa nyakati tofauti, kwa sasa yupo huru tangu alipoachana na Mashujaa FC, Februari 26, 2025, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 3-0 na Singida Black Stars.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zimelidokeza Mwanaspoti kuwa, Baresi ni kipaumbele cha kwanza cha kuiongoza kwa msimu ujao, licha hadi sasa ya kutofanya uamuzi wa mwisho kama wataendelea na Josiah aliyeiwezesha kubaki Ligi Kuu.

“Kipaumbele cha kwanza ni cha kubaki na Josiah lakini uwezekano unaweza ukawa mdogo kwa sababu kuna mahitaji yake ambayo hata msimu uliopita ilikuwa ni ngumu kutimiziwa na uongozi, hivyo ikaleta sintofahamu zaidi,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumzia kuhusu hatima yake ndani ya kikosi hicho, Josiah alisema mkataba wake wa miezi sita umeisha na sasa yupo mapumzikoni, hivyo kama kutakuwa na mazungumzo yoyote basi uongozi utamjulisha, hivyo hawezi kuzungumza tofauti na hilo.

Kwa upande wa Baresi alipotafutwa na Mwanaspoti, alisema kuna ofa mbalimbali ambazo ameanza kuzipokea, ingawa ni mapema kuweka wazi kwa sababu hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa, japo anaheshimu kila mmoja anayethamini uwezo alionao.

Kwa msimu wa 2024-25, Baresi aliiongoza Mashujaa katika jumla ya mechi 22, ambapo kati ya hizo alishinda tano, sare nane na kupoteza tisa, akifunga mabao 17 na kuruhusu 26, akikiacha kikosi hicho kikiwa nafasi ya 11 kwa pointi zake 23.

Josiah aliyejiunga na Prisons, Januari 2, 2025, akitokea Geita Gold, aliiwezesha kumaliza katika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 31 na kucheza ‘playoffs’ za kubaki Ligi Kuu na Fountain Gate iliyomaliza ya 14 kwa kuwa na pointi 29 na kunusurika kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2.

Kichapo hicho cha Fountain, kikaifanya timu hiyo kucheza tena ‘playoffs’ za kubaki dhidi ya Stand United kutoka Championship na kuifunga jumla ya mabao 5-1, hivyo kubaki Ligi Kuu, huku ‘Chama la ‘Wana’ likiendelea kushiriki Ligi ya Championship kwa msimu ujao.

Related Posts