Nyamanzi City, Kundemba FC zaanza vizuri Yamle Yamle Cup

TIMU ya Kajengwa FC imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao Mborimborini FC katika mashindano ya Yamle Yamle Cup yanayoendelea kisiwani Unguja huku yakichezwa kwenye Uwanja wa Mao A na Mao B.

Mechi hiyo iliyochezwa jana Jumatatu Julai 14, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A majira ya saa 10 jioni, Khamis Abdallah wa Kajengwa alianza kufunga bao dakika ya 15, huku Omar Ali akiongeza la pili dakika ya 35.

Katika kipindi cha pili, Nassor Kaboka wa Mborimborini aliipatia bao la kufutia machozi timu hiyo dakika ya 62 huku Mukrimu Nassor wa Kajengwa alikuja kuhitimisha ushindi akiongeza bao la tatu dakika 85.

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa Mao B, ulimalizika kwa Nyamanzi City kutoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Monduli Combine ambapo dakika ya saba Ali Haji Khamis alianza kufunga, akifuatiwa na Omar Salum dakika ya 66 na Siraji Ali Iddi kumalizia bao la tatu dakika ya 90.

Baada ya mechi hizo za kundi A kucheza, msimamo unaonesha Nyamanzi City inashikilia nafasi ya kwanza kwa tofauti ya mabao ikifuatiwa na Kajengwa ambazo zote zina pointi tatu, Mborimborini ya tatu na Manduli ikishika nafasi ya nne.

Kwa upande wa mechi za Kundi C zilizochezwa jana saa 12:30 jioni, Kundemba FC imetoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya S/Kwerekwe FC, mabao yote yakifungwa na Mahmoud Haji dakika ya 20, 42 na 90.

Manyalu City iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Melitano City. Mabao ya Manyalu City yalifungwa na Mohammed Mussa (dk 31), Juma Suleiman (dk 70) na Fereji Salum (dk 84), kwa upande Melitano City mabao yote yalifungwa na Omar Thani dakika ya 7 na 33.

Msimamo wa Kundi C nafasi ya kwanza inashikiliwa na Kundemba, Manyalu ya pili, Melitano ya tatu na S/Kwerekwe ya nne.

Mashindano hayo yataendelea leo jioni kwa kuchezwa mechi za Kundi B ambapo Miembeni City itakutana na Al-Qaida FC na JKU Academy itavaana na Mambosasa. Kwa  upande wa Kundi D, Melinne City itakabiliana na Muembe Makumbi na Luxury FC dhidi ya Kinazini.

Related Posts