Yanga yampa miwili kiungo Mkenya

UONGOZI wa kiungo Lydia Akoth raia wa Kenya, umesema mchezaji huyo amenunuliwa na Yanga Princess baada ya mkataba wa mkopo wa miezi sita kumalizika.

Kiungo huyo alisajiliwa dirisha dogo la msimu uliomalizika akitokea Kenya Police Bullets FC ya nchini kwao na sasa ni mchezaji halali wa Yanga Princess kuanzia Agosti Mosi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.

Uongozi huo ulisema: “Baada ya kutumika sehemu ya pili ya msimu wa 2024-25 kwa mkopo katika klabu ya Yanga Princess, tungependa kuthibitisha kwamba mchezaji wetu Akoth amejiunga jumla na timu ya Tanzania, Yanga Princess akitokea Kenya Police Bullets FC,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:

“Lydia ni kiungo anayeweza kucheza katika maeneo mengi, atajiunga rasmi na timu yake mpya kuanzia Agosti Mosi, 2025 kwa kipindi cha miaka miwili, tunamtakia kila la kheri.”

Ndani ya kipindi kifupi alichocheza Yanga Princess, alionyesha kiwango bora na kuwa miongoni mwa majina yaliyokuwa yanatajwa na mashabiki wa timu hiyo waliokuwa wanamtazama.

Akiwa Kenya Police, alikuwa mchezaji muhimu kwenye timu hiyo ambayo msimu wake wa kwanza aliiwezesha kuchukua ubingwa likiwa taji la kwanza kwa timu hiyo akifunga mabao manane na asisti 10 kwenye mechi 18.

Kiwango alichoonyesha kilimfanya anyakue tuzo ya mchezaji bora wa msimu 2023/24 (MVP) mbele ya Maximilla Robie wa Kibera Queens na Rebecca Okwaro.

Related Posts