Bado elimu ya watu wazima haieleweki kwa wengi

Wengi wanaojitambulisha kuwa na uhusiano na elimu hii, hukutana na mshangao na maswali kama Elimu ya Watu Wazima bado ipo?”, “Ni nini hasa Elimu ya Watu Wazima  au  ndiyo hiyo  ngumbaru?

Maswali haya kutoka kwa watu mbalimbali na baadhi yao wakiwa na uelewa wa masuala mbalimbali hasa ya elimu, yanaleta tafakuri kuhusu uelewa wa aina hii ya elimu nchini.

Agosti mwaka huu,  Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW),  itaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Hata hivyo, dhana ya Elimu ya Watu Wazima bado haieleweki vizuri kwa watu wengi.

Wengi wanaojitambulisha kuwa na uhusiano na elimu hii, hukutana na mshangao na maswali kama Elimu ya Watu Wazima bado ipo?”, “Ni nini hasa Elimu ya Watu Wazima  au  ndiyo hiyo  ngumbaru?

Maswali haya kutoka kwa watu mbalimbali na baadhi yao wakiwa na uelewa wa masuala mbalimbali hasa ya elimu, yanaleta tafakuri kuhusu uelewa wa aina hii ya elimu nchini.

Dhana ya elimu ya watu wazima si mpya katika sekta ya elimu, bali ni ya kihistoria katika maisha ya binadamu. Mizizi yake ilianzia Ugiriki ya kale kupitia wanafalsafa kama Socrates, Aristotle, Heraclites na Seneca, waliosisitiza kujifunza maisha yote.

Fikra hizi ziliendelezwa na wanamapinduzi wa kijamii kama Komensky na Krupska.

Elimu ya watu wazima ilishamiri katika karne ya 18 na 19 kufuatia mapinduzi ya viwanda na ongezeko la uhitaji wa wafanyakazi wenye ujuzi.

Hapo ndipo zilipoanzishwa taasisi kama vyuo vya wafanyakazi, vyama vya kielimu, shule za bweni kwa watu wazima, elimu masafa, vyuo vya maendeleo ya wananchi na upanuzi wa vyuo vikuu.

Wakati Tanzania inapata uhuru mwaka 1961, takriban asilimia 75 ya wananchi hawakujua kusoma na kuandika.

Mwalimu Julius Nyerere alisisitiza kuwa maendeleo hayawezekani bila watu kupata elimu. Hivyo, mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watu wazima yakapewa kipaumbele katika ujumbe wa kisiasa, na Serikali ikaanzisha programu mbalimbali za kuimarisha elimu ya watu wazima. 

Programu mbalimbali ziliendeshwa kama sehemu ya elimu ya watu wazima, zikiwemo: “Kupanga ni Kuchagua ya miaka ya 1960 iliyolenga kueleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano; “Uamuzi ni Wako” (1970) kwa maandalizi ya uchaguzi; “Muda wa Kusherehekea” kwa kuimarisha utambulisho wa taifa; na “Mtu ni Afya, Chakula ni Maisha” (katikati ya miaka ya 1970) iliyofundisha kuhusu magonjwa ya kuambukiza na njia za kujikinga.

Katikati ya miaka ya 1970, Serikali ilianzisha Mpango wa Elimu ya Wafanyakazi uliolenga kuongeza elimu na ufanisi kazini. Programu zake zilihusisha kusoma na kuandika, kisomo cha kujiendeleza, mafunzo ya ufundi na elimu ya jumla.

Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilianzishwa miaka ya 1970 kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi wakati huo, vikilenga hasa kwa wale walio na elimu ya msingi. Vyuo hivi vilianza rasmi mwaka 1976 na viliwezesha elimu ya jumla na ufundi kwa ajili ya maendeleo vijijini.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ilianzishwa mwaka 1960 kama kitengo cha masomo ya ziada katika Chuo cha Makerere chini ya Chuo Kikuu cha London. Baadaye, TEWW ikawa taasisi ya kujitegemea iliyoundwa chini ya Sheria ya Bunge Na. 12 ya 1975, na ikafanya kazi chini ya Wizara ya Elimu ya Taifa.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizounda taasisi ya elimu ya watu wazima ikiwa na jukumu la; kutoa elimu bora kwa watu wazima na elimu endelevu nje ya mfumo rasmi; kushiriki katika shughuli za utafiti zinazochangia maendeleo ya elimu ya watu wazima.

Pia kutoa mafunzo kwa waelimishaji na wawezeshaji wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na kuwezesha jamii kupitia elimu.

Kupitia TEWW, Serikali imeanzisha programu kadhaa za kitaifa za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi kama vile Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA) ulioanzishwa mwaka 1993 ili kuongeza upatikanaji wa elimu msingi kwa watu wazima na vijana waliokosa fursa hiyo. Ujifunzaji unafanyika kwa mbinu ya ‘riflekti’ inayotumia vielelezo shirikishi kuibua dhana za kusoma, kuandika, na hesabu, na kuhamasisha majadiliano ya kutafakari na kutatua changamoto za jamii.

Pia kuna Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA) uliaonzishwa mwaka 1999, ili  kutoa fursa kwa watoto waliokosa kuanza elimu ya msingi rasmi. Programu imegawanyika makundi mawili: kundi la kwanza ni watoto wa miaka 8–13 wanaoanza masomo kwa njia isiyo rasmi kabla ya kujiunga na mfumo rasmi, na kundi la pili ni vijana wa miaka 14–18 wanaopata elimu ya msingi kwa miaka mitatu na kisha kufanya mtihani wa Taifa.

Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio nje ya Shule (MECHAVI) 2018. Programu hii ilianzishwa mwaka 2018 na inatoa elimu ya fursa ya pili kwa vijana nje ya shule wenye umri kati ya miaka 14 hadi 19. Mpango huu unatoa seti kuu za ujuzi nne: ujuzi wa ufundi, ujuzi wa ujasiriamali, ujuzi wa maisha, na ujuzi wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala. Programu hii inawalenga vijana wasio shuleni na watu wazima ambao walikosa fursa za kuendelea na shule ya sekondari katika mfumo rasmi au wale wanaotafuta sifa za elimu ya sekondari, lakini hawawezi kujiunga na elimu ya sekondari katika mfumo rasmi.

Elimu ya watu wazima dhana pana

Dhana ya elimu ya watu wazima ni pana sana na hasa inapoangaliwa kama ujifunzaji usio na ukomo.

TEWW kupitia programu mbalimbali kwa kusaidiana na wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wadau mbalimbali kama vile DVV International, Unicef, CANFED na wengineo,  wanafanya jitihada za kutimiza malengo ya Maendeleo Endelevu  hasa lengo Namba 4.6, ambalo linakusudia kuhakikisha kuwa vijana na watu wazima wote wanapata elimu ya kusoma na kuandika na hesabu ifikapo mwaka 2030.

Miaka 50 ya TEWW  ni ushahidi wa dhamira ya Taifa katika kuwajengea wananchi uwezo wa kujifunza katika hatua zote za maisha.

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado ipo haja ya kuongeza uelewa wa dhana ya elimu ya watu wazima kwa umma, na kuhakikisha kuwa elimu hii inajumuishwa kikamilifu katika mifumo ya kitaifa ya elimu na maendeleo.

Matteo Mwita ni mdau wa elimu ya watu wazima.

Related Posts