Tunahitaji viongozi wenye utu, wanaojali utu, wanaotolea maisha yao kwa masilahi ya wote.
Tukiwa na utawala unaojali Katiba yetu, sheria na utu wa watu, hakika ukatili kama uliotokea huko Geita utapungua.
Pierre Trudeau, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Canada kuanzia 1968 hadi 1984, aliwahi kusema:
‘’Kujenga taifa si kama wafalme (pharaohs) wa Misri walivyojenga mapiramidi ambayo mpaka sasa ni vivutio vikubwa vya utalii, bali ni kila siku kujenga uadilifu unaokubalika katika jamii hiyo.’’ (A country is something that is built every day of certain shared values).
Pia Mwalimu Julius Nyerere ameandika: ‘’Ukweli ni kwamba maendeleo maana yake ni maendeleo katika utu wa wananchi. Kujenga mabarabara, majengo ya fahari, kuongeza mavuno mashambani na mengine ya aina hiyo, si maendeleo. Hivi ni vichocheo vya maendeleo.’’
Mwalimu anatoa mfano wa mapiramidi ya Misri, barabara na madaraja ya Ulaya ambayo mpaka leo ni ya kustaajabisha, lakini kwa sababu maendeleo hayo hayakwenda sambamba na maendeleo ya utu, falme hizo za Ulaya zilianguka. Haya yalikuwa maendeleo ya vitu si maendeleo katika utu.
Nimekumbuka maneno haya ya busara niliposoma katika gazeti hili Julai 5, 2025, kuhusu kijana mmoja, Enock Mhangwa (25) mkazi wa kijiji cha Uyovu wilayani Bukombe mkoani Geita, alivyopoteza maisha baada ya madai kwamba alipigwa na ofisa mtendaji na askari mgambo wawili.
Niliona video iliyotembea sana mitandaoni ikionyesha mubashara kijana huyo akipigwa na fimbo na watu wawili wakipokezana.
Katika video hiyo nilimuona mwingine amesimama kando akiangalia kinachoendelea pale.
Kijana amefungwa mikono nyuma, yupo hapo chini akilia na kupiga mayowe kwa maumivu anayopata, wale wanaendelea kumchapa kama vile hawasikii kilio chake, wanamchapa popote pale mwilini.
Roho yangu iliumwa sana kuona mwanadamu mwenzangu, mtoto wangu, jirani yangu, mwananchi mwenzangu, akifanyiwa ukatili wa kiwango hicho.
Nikawa najiuliza: je, hawa wachapaji ni watu wa aina gani? Je, hawasikii kilio cha huyu kijana? Je, roho zao zimekufa au zi hai?
Ni mtu wa aina gani anaweza kutembeza kichapo cha aina hii bila kujali anavyolia mwanadamu mwenzake?
Napata maswali haya si kutokana tu na tukio hilo, lakini pia ni kutokana na matukio ya aina hii yanayoongezeka nchini na duniani kwa ujumla.
Tunashuhudia ukatili wa kutisha katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Si siri kwamba watu wanatekwa, wanapotezwa na wengine kuuawa tena baada ya mateso yasiyoelezeka.
Tunaona ukatili katika familia zetu. Tunasikia kwamba mwanafunzi fulani amepoteza maisha kutokana na kipigo cha mwalimu wake.
Katika hospitali zetu na vituo vya afya, tumeona ukatili ukitembezwa kwa wagonjwa, tumesikia mgonjwa akifa baada ya kusubiri huduma ambayo hakupewa.
Ukatili ni mwingi, roho za mawe na chuma zinaongezeka. Tujiulize: tunakwenda wapi? Je, tumefikia mahali pale maandishi matakatifu yanasema: wana macho lakini hawaoni, wana masikio lakini hawasikii?
Nipitapo njiani katika kata yetu nasikia watoto wakilia kwa vipigo vya wanaojiita wazazi, mtoto analia kwa mateso, na huyu mzazi, ambaye anapaswa kulinda masilahi ya mtoto wake, anaongeza kipigo na kumtupia matusi ambayo hayatamkiki hapa. Unajiuliza: tumefikaje hapa? Haya ni maendeleo ya staili gani?
Je, huyu mtoto baadaye atakuwa mtu wa aina gani? Hivi baadaye, huyu mtoto anayekuzwa kwa kipigo mara kwa mara, baadaye ukubwani akamgeukia huyu mzazi wake na kumtembezea kipigo cha kutosha, huyu mzazi atashangaa kupata kipigo hicho? Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ni msemo wa Kiswahili.
Siku moja nilikuwa darasani katika chuo kikuu kimoja hapa nchini nikifundisha somo la falsafa na maadili. Wanafunzi wangu walikuwa katika ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu (M.A. and Ph.D. students).
Tukazungumza siku hiyo kuhusu wajibu wa wazazi katika kulea watoto wao. Mmoja akasema kwamba yeye anatumia fimbo kulea watoto wake ili kuwaweka njia sahihi.
Kwa vile mimi si muumini wa uchapaji wa aina yoyote, niliona hapa fursa ya kujenga hoja kwamba uchapaji wa watoto, wenza wa ndoa, wanafunzi na wale wanaovunja sheria, si njia sahihi ya kulea watoto, wanafunzi na kujenga taifa imara.
Tukawa na mjadala mzito katika darasa hili lililokuwa na wanafunzi kama 120 hivi. Zaidi ya nusu darasani walijenga hoja kwamba fimbo ni njia nzuri ya kulea watoto na wanafunzi. Waliobaki wakapinga hoja hiyo.
Baada ya wiki moja mmojawapo wa hao wanafunzi walioshabikia uchapaji, akaomba kutoa mawazo yake kuhusu uchapaji nyumbani mwake.
Akasema yeye kwa muda mrefu alitumia fimbo kama mwarobaini wa kujenga nidhamu nyumbani mwake.
Ikawa kwamba baada ya majadiliano yetu darasani kuhusu uchapaji wa watoto, alifanya tafakari nzito, na akachukua fimbo yake maalum aliyokuwa anaitumia kushusha kipigo kwa watoto wake, akaikatakata vipande na kuitupilia mbali mbele ya watoto wake.
Siku iliyofuata alipofika nyumbani kutoka kazini alishangaa watoto kumkimbilia mlangoni na kumpokea baba kwa upendo.
Hapo awali ilikuwa akifika nyumbani watoto walipotea kusikojulikana, walijificha. Kwa kifupi walimwogopa baba yao. Sasa wamegeuka, wamekuwa rafiki zake.
Huyu mwanafunzi akafikia tamati ya hoja yake kwa kusema: ‘’Tangu niache kuwachapa watoto wangu, tumekuwa na ukaribu zaidi nyumbani na ni katika chungu hicho cha ukaribu nimeweza kuwalea watoto wangu kwa mafanikio zaidi.’’
Akamalizia: ‘’Huwezi kumlea vizuri mtoto anayekuogopa. Malezi sahihi ni katika ukaribu kati ya mzazi na mtoto, mwalimu na mwanafunzi.’’
Hivyo pia malezi sahihi ya taifa si katika watawala na vyombo vya usalama kutembeza vipigo, au kutawala kwa virungu, risasi na mabomu. Njia hizi za malezi na utawala hujenga taifa la watu wakatili wasio na utu.
Nikirudi katika lile tukio la kumpiga kijana wetu, naamini kwamba waliompiga hadi kufa ni watu waliopigwa sana nyumbani au shuleni.
Katika malezi hayo ya vipigo, walijifunza kwamba kipigo ndiyo njia sahihi ya kumwadhibu mkosaji. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Hapana, tutoke huko tuende mbele katika kujenga taifa la watu waadilifu, wanaowajali wenzao.
Ni sahihi kusema kwamba tunahitaji mifano mizuri kutoka kwa viongozi wetu wa aina zote: viongozi wa siasa, wa Serikali, wa dini, wa taasisi mbalimbali.
Tunahitaji viongozi wenye utu, wanaojali utu, wanaotolea maisha yao kwa masilahi ya wote. Tukiwa na utawala unaojali Katiba yetu, sheria na utu wa watu, hakika ukatili kama uliotokea huko Geita utapungua.