Mbeya. Ili kunusuru vyanzo vya maji na kuongeza hali ya uzalishaji wa chakula, wataalamu wameshauri nchi za Afrika Mashariki kushirikiana kimkakati kuzuia shughuli za kijamii katika maeneo hayo.
Pia, wameshauri namna ya kuepukana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza kilimo chenye tija ni kuweka mazingira mazuri kwa wakulima na kuwapa mbinu za matumizi sahihi ya teknolojia katika kutumia kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua pekee.
Akizungumza leo Julai 15 katika mwendelezo wa kongamano kujadili chakula, nishati na maji kwa nchi tisa lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Mkurugenzi wa umwagiliaji nchini Kenya, Daniel Odero amesema kwa sasa vyanzo vya maji vinapungua kutokana na shughuli nyingi za kijamii.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, nchi zinaunda Afrika Mashariki zinapaswa kuwa na ushirikiano wa pamoja na kuweka mikakati ya kuzuia shughuli hizo kwani chakula na nishati vinahitaji nguvu ya maji.

Washiriki kutoka mataifa mbalimbali wakiwa katika kongamano la kujadili Chakula, Nishati na Maji linaloendelea jijini Mbeya.
“Nishati na chakula vinahitaji sana maji, kwa kuwa hakuna zao litastawi bila kuwa na maji, kwa sasa vyanzo vingi maji yanakauka hivyo ili kuleta ustawi na kuzalisha kwa tija lazima nchi zetu zizuie shughuli kwenye vyanzo hivi,” amesema Odero.
Kwa upande wake meneja na msimamizi wa kongani ya Mbarali inayohusisha baadhi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Abdalah Hamad amesema kilimo cha umwagiliaji kikiwezeshwa kinaweza kuleta tija kwa wakulima badala ya kutegemea zaidi mvua pekee.
Amesema kwa sasa Serikali inaonesha dhamira kubwa kwenye uwekezaji katika maeneo ya nishati, maji na chakula akibainisha taasisi za fedha zimekuwa sehemu ya kufanikisha teknolojia hiyo kwa kutoa mikopo.
“Bado safari ni ndefu lakini ipo dalili nzuri za kuweza kufikia malengo kwa kuwa tunaona Serikali inavyowekeza nguvu kwa kushirikiana na wadau, iwapo tutafanikiwa, tutakuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija,” amesema Hamad.
Naye Bibi Shamba, Ritha Laizer kutoka Taasisi ya Itec, amesema kumekuwapo na changamoto katika kwa wakulima haswa baadhi ya mazao kushambuliwa na visumbufu mimea, akieleza kuwa wao kama wataalamu wamekuwa wakijikita kutoa elimu kwa wakulima shambani.
“Kongamano hili linaweza kuleta mabadiliko kwakuwa wataalamu wengi wanaeleza changamoto, sababu na mipango mikakati ya kukabiliana nayo, Tanzania tukiwa wenyeji tunaweza kunufaika moja kwa moja,” amesema Ritha.