MCT yatimiza miaka 30 ikiwatambua Nyerere, Mwinyi kuhimiza uhuru wa habari

Arusha. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema kumekua na mabadiliko ya sheria, sera na utashi wa kisiasa kuviwezesha vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Amesema hayo leo Jumanne Julai 15, 2025 wakati akifungua kongamano la pili la mabaraza ya Habari barani Afrika (Nimca) iliyofanyika jijini hapa kuwa sekta ya habari ina mchango muhimu katika kusukuma ajenda ya maendeleo endelevu kwa wananchi.

“Juhudi zenu kufanya kongamano hili la wadau kutoka barani Afrika ni ushahidi kuwa mmejitoa kikamilifu kusukuma ajenda ya mazungumzo yenye tija yanayohusu uandishi wa habari, uhuru wa vyombo vya habari na mwasiliano,vilevile umuhimu wa majukumu ya vyombo vya habari katika kuchagiza maendeleo endeleo endelevu,”amesema Dk Mpango

Amesema majukumu ya mabaraza ya habari ulimwenguni kote ni kusimamia mienendo ya taasisi za vyombo vya habari kwenye maeneo husika kwa kuhakikisha uwajibikaji na maadili ya sekta hiyo.

Aidha,ameongeza kuwa mabaraza ya habari yanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoathiri taaluma, uadilifu na ufanisi wake jambo linalozorotesha kuaminika kwenye jamii na kusabisha kusambaa kwa taarifa zisizo na ukweli na taarifa za uchochezi kupitia mitandao ya kijamii.

“Vyombo vya habari imara vinategemea umathubuti wa kisheria na mfumo wa kisheria wa taasisi kuheshimu uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari ambayo inahitaji kujengewa uwezo kwenye mazingira ya kuwa na uwiano wa habari zenye maslahi kwa umma,uhuru na misingi ya kimaadili,”amesema Dk.Mpango

Amesema serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya habari walifanyia mabadiliko sheria ya vyombo vya Habari kwa lengo la kuonisha na matakwa ya Katiba,viwango vya kimataifa vya Haki za Binadamu na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia.

Makamu wa Rais ameongeza kuwa moja ya maeneo yaliyofanyiwa mabadiliko ni kukiondoa kifungu kilichokua kinampa mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kutoa adhabu kwa waandishi, kurahisisha upatikanaji na kuhuisha leseni na kujenga mazingira ya uwazi.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya dhati kuviwezesha vyombo vya habari kiuchumi ikiwemo kulipa madeni ambayo vyombo vya habari vinaidai serikali.

Amesema katika kukabiliana na changamoto za vyombo vya habari nchini wataalamu wa habari waliweka Azimio la Dar es Salaam ambalo lililenga pamoja na mambo mengine uhuru wa kupata habari na uwajibikaji wake na haki ya kupata taarifa.

Katika kongamano hilo,Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari nchini (MCT) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Nimca, Ernest Sungura amesema katika kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, wametambua mchango wa marais wa awamu ya Kwanza na pili wa Tanzania katika kukuza maendeleo ya Habari nchini.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipokea tuzo kwa niaba ya Hayati Ali Hassan Mwinyi na kusema kuwa tuzo hiyo ni muhimu kwa kutambuliwa kwenye uongozi wake namna aliweka mazingira mazuri kwa sekta ya habari.

Kwa upande wake Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa hayati mwalimu Nyerere alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya baba yake.

Related Posts