Takukuru yachunguza malalamiko 11 rushwa dhidi ya watiania wa ubunge CCM Kilimanjaro

Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imeeleza kuwa imepokea malalamiko 11 yanayohusu vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya watiania wa ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne Julai 15, 2025 na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo wakati akizungumza na watia nia wa ubunge kupitia CCM kutoka Jimbo la Vunjo na Moshi Vijijini kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chama hicho.

Chaulo amesema, malalamiko hayo yameanza kufanyiwa kazi, huku baadhi ya watuhumiwa tayari wakiwa wamehojiwa ili kufahamu undani na ukweli wa tuhuma zinazowakabili.

“Tumepokea malalamiko 11 katika ofisi yetu ya Takukuru, yanayohusiana na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watiania ya ubunge ndani ya CCM,  tunaendelea kuyafanyia kazi na kuyachakata ili tuone ukweli wa malalamiko hayo,” amesema Chaulo.

Ameongeza kuwa; “Tumeanza kuyachakata malalamiko hayo ili kubaini ukweli. Kipindi hiki cha uchaguzi malalamiko mengine ni ya watu kutengenezeana tuhuma ambazo sizo sahihi, lakini tupo makini katika kuhakikisha kila tuhuma tunayoipata tunaifanyia kazi kwa undani zaidi ili tuweze kupata uthibitisho kabla ya kufika kwenye hatua nyingine.”

Amesema, Chama Cha Mapinduzi kimeweka taratibu za maadili, lakini wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakikiuka utaratibu huo kutokana na masilahi yao binafsi jambo ambalo haliwezi kufumbiwa macho au kuvumiliwa na Takukuru.

Amesema  kiongozi anayeingia madarakani kwa rushwa hataweza kuwasaidia wananchi wake na kudai kuwa wapo baadhi ya viongozi waliokuwa madarakani ambao baada ya kupata nafasi hizo walipotea moja kwa moja na sasa wamerudi kuomba tena kurejea katika nafasi hizo huku wakitangaza wamekuja  na fedha.

“Takukuru haitakubali kuona utaratibu unavunjwa. Yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo vya rushwa tutamchukulia hatua na mpaka sasa tunao baadhi ya watiania ambao tunaendelea kukamilisha uchunguzi ili tuweze kuwachukulia hatua, tunajua vipo vikao vinafanyika usiku wa saa nane  sio kwamba hatujui, tunajua na tunafuatilia. Lakini, niwaombe mtupe ushirikiano ili kudhibiti vitendo hivi,” amesema Chaulo.

Amesema baada ya kukamilisha uchunguzi wao, wapo baadhi ya watiania watafikishwa mahakamani na kwenye ngazi ya chama ili kueleza wazi walivyofanya na kuvunja kanuni za chama kabla ya uteuzi kufanyika ili wasiteuliwe na chama kugombea nafasi hizo.

Aidha, Chaulo amesema Takukuru imepanga kukutana na watiania wote wa ubunge katika mkoa huo pamoja na wanaowania nafasi za udiwani ili kuwaelimisha kuhusu madhara ya rushwa na kuwapa onyo  dhidi ya kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ya uchaguzi.

Baadhi ya watia nia ya ubunge  CCM Jimbo la Vunjo na Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, wakiwa kwenye kikao na Takukuru.



“Rushwa ni adui wa haki na maendeleo. Tumeamua kuwakumbusha wajibu wao kabla ya kuanza kwa kampeni na mchakato mzima wa uchaguzi ili kila mmoja awe na ufahamu wa kile anachopaswa kufanya,” amesisitiza.

Akizungumzia tuhuma hizo, Wilhard Kitaly ambaye ni mtiania Moshi Vijijini, amesema ni vyema wale wanaohusika na vitendo vya rushwa wakatajwa na kuwekwa wazi ili kuwa fundisho kwa wengine.

“Elimu hii ni nzuri tunashukuru sana, lakini umesema wapo watu wameshafikishwa kwenu wakituhumiwa kujihusiaha na vitendo vya rushwa, tunaomba watu hawa watajwe. Lakini, pia elimu hii iwafikie pia wajumbe ili kila mmoja atambue ni kosa kupokea au kutoa rushwa,” amesema.

Naye Joseph Mlay mtiania Vunjo ameshauri baada ya CCM kurudisha majina matatu ya watiania watakaogombea katika kura za maoni, taasisi hiyo ikutane nao ili kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea mchakato wa kura za maoni.

Kwa mujibu wa Takukuru, hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanyika kwa uwazi, haki na kuzingatia misingi ya maadili ya uongozi.

Katika kikao hicho Takukuru ilitarajia kukutana na  watiania 44 wa majimbo ya Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Vunjo,  lakini waliohudhuria ni watiania 13 kutoka majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo.

Related Posts