Walimu 941 Nyanda za Juu Kusini wanolewa mafunzo ya Tehama, RC Malisa atoa neno

Rungwe. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya (RC), Beno Malisa ameishauri Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia  kuanzisha programu  maalumu ya elimu ya uwekezaji kwa watumishi wa umma wakiwepo walimu.

Malisa amesema leo Julai 15, 2025 wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa walimu wa Shule za Sekondari  941 kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mafunzo hayo yamefadhiriwa na Serikali kupitia mkopo nafuu wa Benki ya Dunia chini ya  mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (Sequip) na kuhusisha mikoa saba ya  Mbeya, Iringa, Songwe, Ruvuma, Katavi na Njombe.

“Nishauri wizara kutupia jicho suala la elimu ya uwekezaji kwa watumishi wa umma wakiwepo walimu ili kuwajengea kesho iliyo bora mara baada ya kustaafu kwa kuishi maisha mazuri,”amesema.

Malisa amesisitiza ni wakati sasa walimu kujiwekeza ili kujiimarisha katika maisha ya baadaye  kwa lengo na kuishi  maisha bora  baada ya kuachana na utumishi serikalini.

“Ni muda mzuri kwa watumishi wa umma  kuwekeza nasema hivyo kwa sababu  Mimi ni mtoto wa mwalimu ,lakini ni jambo jema serikali kuona umuhimu wa kutoa elimu ya uwekezaji,” amesema.

Walimu wa Shule za Sekondari Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ,Beno Malisa (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo  Teknolojia  ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kupitia mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari  (SEQUIP), yaliyoanza leo Julai 15,2025 katika Chuo cha Uwalimu Mpuguso  Wilaya ya Rungwe mkoani hapa. Picha na Hawa Mathias



Katika hatua nyingine, Malisa ameonya walimu kutokuwa chanzo cha mmonyoko wa maadili kwa wanafunzi na  badala yake wawe chachu ya kutimiza wajibu na kulinda heshima ya taaluma na taifa kwa ujumla.

“Asilimia kubwa ukifuatilia kwenye vyombo vya dora unakutana na mashauri ya mengi ya  walimu kuwa chanzo cha mmonyoko wa maadili sasa umefika wakati kugeukia kutoa taaluma bora katika ufundishaji,” amesema.

Malisa pia amesisitiza walimu walionufaika na fursa ya mafunzo ya tehama wakawe chachu ya darasa  kwa wengine ili kuwezesha serikali kupitia Wizara ya Elimu kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kuhusu ufundishaji wa tehama ,Malisa amesema wakakubali kukosolewa na wanafunzi wanao kwenda  kuwafundisha kufuatia wao kuwa mbele zaidi katika matumizi ya teknoloji .

“Kizazi cha sasa watoto wetu wamepiga hatua sana katika matumizi ya teknolojia ,sasa mkatumie lugha nzuri katika ufundishaji ,kukubali kukosolewa na kutotumia ubabe.,”amesema.

Mratibu wa Mradi wa Kuboresha  Elimu ya Sekondari  (Sequip), Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Robert  Msigwa amesema lengo la mradi huo ni kuwajengea uwezo walimu 914 katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

“Mradi huu utahusha mikoa saba kutoka Kanda hii,lakini pia Serikali imeboresha miundombinu  ya shule kongwe nchini sambamba na mifumo ya Tehama ambayo itawezesha mwanafunzi kujifunze eneo lolote nje ya Shule,” amesema.

Katika hatua nyingine amesema katika kuboresha mitaala ya elimu  walimu 13,272 wamerejeshwa katika mfumo usio rasmi kwenye vituo vya elimu ya watu wazima.

Sambamba hilo Msigwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Tamisemi  kwa mwaka 2024/25 imechapisha vitabu vya masomo mbalimbali milioni 6.8 na kusambaza katika Shule za Sekondari.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari  Maluja iliyopo Mkoa wa Katavi, Mussa Thomas ameshauri serikali inapokuja na mpango huo iwekeze katika upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika katika maeneo ya vijijini.

“Kuna maeneo  nishati ya umeme ni changamoto  ili kufikia malengo serikali iweze kuboresha  upatikanaji wa  nishati ya umeme wa uhakika vinginevyo elimu ya mipango ya elimu ya  tehama haitafanikiwa, “amesema.

Related Posts