Wanafunzi waiomba Serikali iwalinde wanapotoa taarifa vitendo vya ukatili

Iringa. Wanafunzi mkoani Iringa wameiomba Serikali kuwalinda dhidi ya vitisho na madhara wanayoweza kuyapata endapo wataamua kuripoti ukatili wanaofanyiwa majumbani, hasa kutoka kwa wazazi au walezi.

‎Wanafunzi hao wameyaeleza hayo kwa njia ya kuuliza swali Julai 14, 2025 katika mkutano uliohusisha wadau wa usafirishaji, ustawi wa jamii na wanaharakati wa haki za watoto uliofanyika katika viwanja vya Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Iringa kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

‎“Ikiwa tutatoa taarifa za ukatili tunafanyiwa nyumbani, je Serikali itatusaidiaje kwa wazazi na walezi wetu maana tunapata vitisho kutoka kwa familia zetu na ukiwaza mzazi ndio anayenipatia msaada,” amesema Nagi Ismaili, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Miyomboni mkoani Iringa.

‎Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakionyesha kumuunga mkono mwanafunzi huyo kwa kupiga makofi.

‎ ‎Akizungumzia hali hiyo na kujibu swali lililoulizwa,  Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa, Martin Chuwa amesema Serikali kupitia mifumo yake ya kisheria, inalinda watoto wanaotoa ushahidi dhidi ya ukatili wanaofanyiwa.

‎“Mara nyingi tunaiomba mahakama kutoa amri ya kuwaondoa Watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili kwa wazazi au walezi ili kuhakikisha usalama wao na uhai wao unaendelea kuwepo,” amesema Chuwa.

‎Katika hatua nyingine Chuwa ameongeza kuwa Sheria ya Mtoto inaanza kumlinda mtoto tangu anapokuwa tumboni, na kwamba jamii inapaswa kufahamu kuwa mahusiano ya wawili siyo ya watu binafsi pekee, bali yana athari kwa taifa zima hasa yanapohusisha watoto wadogo.

‎Mratibu wa Dawati la jinsia na Watoto, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Faidha Suleiman ametoa wito kwa madereva wa bajaji na bodaboda kuepuka kabisa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.

‎ACP Faidha amesisitiza kuwa hata kama mwanafunzi amekubali, kisheria bado ni mtoto na mhusika anaweza kuchukuliwa hatua kali.

‎“Miongoni mwa vichochezi vya ukatili ni ulevi, mmomonyoko wa maadili na ndizo tunazopambana nazo kila siku,” amesema ACP Faidha.

‎Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi amesema kuwa juhudi zinaendelea kufanywa kwa kushirikiana na mashirika ya kijamii, shule na viongozi wa dini ili kuwaelimisha wazazi na walezi kuhusu haki za watoto.

‎Akizungumzia takwimu za vitendo vya ukatili, Kamanda Bukumbi ameeleza kuwa waathirika wa kwanza ni watoto, wakifuatiwa na wanawake na mwisho ni wanaume.

‎Mwenyekiti wa Wasafirishaji wa Bodaboda mkoani Iringa, Zuberi Mapila amesema kuwa katika kuhakikisha bodaboda hawahusiki na ukatili, wameacha kujihusisha na biashara haramu au tabia zinazoweza kuhusishwa na uhalifu wa kijinsia.

‎”Sisi kama bodaboda tumejipanga kuhakikisha hatutumiki kama chombo cha kuwadhuru watoto,” amesema Mapila.

‎Katibu wa Madereva Bajaji Miyomboni Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Khery Ngumbi amewaomba wazazi kuwapa watoto wao nauli ya kutosha ili kuepuka kuwaweka kwenye mazingira hatarishi.

‎Baadhi ya wazazi na walezi kutoka mkoani Iringa wamekiri kuwa huona aibu pale wanapotoa ushahidi dhidi ya wenzake au ndugu waliohusika na ukatili, hali inayorudisha nyuma juhudi za kupambana na tatizo hilo huku wakiiomba jamii ya mkoa huo kukemea vitendo vya ukatili.

Related Posts