ACT Wazalendo yawapa ujumbe Watanzania kuhusu uchaguzi mkuu

Rufiji. Kundi la pili la viongozi wa ACT Wazalendo, limehitimisha ziara ya siku 15 operesheni ya majimaji Oktoba linda kura, huku likitoa ujumbe kwa Watanzania likiwaeleza yaliyojitokeza katika chaguzi za mwaka 2019/20 na 2024 yasiwakatishe tamaa bali wajitokeza kushiriki Uchaguzi Mkuu

Katika chaguzi za serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wa mwaka 2019 vyama vya upinzani waliulalamikia mchakato huo wakidai haikuwa rafiki, kabla ya hawajakaa sawa hali hiyo ikajitokeza tena kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 ambapo asilimia kubwa wabunge wa CCM walishinda majimbo pamoja na kata.

Katikati ya sintofahamu hiyo, hali ya mambo ikarejea tena katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024, ambapo upinzani walilalamika wakidai haikuwa wa kidemokrasia ndio maana kata, vijiji na vitongoji vilinyakuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).


Licha ya hayo yote kutokea Chama cha ACT Wazalendo, kimetoa ujumbe wa kuwasihi Watanzania kutoka tamaa na yaliyojitokeza, badala yake washiriki uchaguzi wa Oktoba ili kufanya mabadiliko kuanzia udiwani hadi urais.

Kundi la kwanza lililojikita kanda ya ziwa liliongozwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu akiambatana na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho, wakiwemo wajumbe wa kamati kuu ambapo walihitimisha ziara yao jana Jumatatu Julai 14, 2025 jijini Dar es Salaam.

Wakati kundi la pili liliongozwa na kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo (Bara) Esther Thomas limehitimisha ziara yake katika Jimbo la Rufiji baada ya kutembelea mikoa ya kusini.


Akiwahutubia wananchi wa Rufiji leo Jumanne Julai 15, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), eneo la Ikwiriri, Zitto ameanza kwa kuwashukuru Watanzania kwa namna walivyojitokeza kuwaunga mkono katika ziara hiyo.

“Yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita ni mambo ambayo yanatufunza namna ya kukabiliana na changamoto zinazoathiri haki zetu.Yasiye mambo ya kuturudisha nyuma, bali yawe mambo ya kutupanga upya,” amesema.

“Ndugu wananchi mambo yaliyojitokeza yanatufanya tuwe na nguvu ya kukabiliana na CCM, ndio maana ACT Wazalendo imeamua kushiriki uchaguzi licha ya madhila yaliyojitokeza,” amesema Zitto.


Amefafanua ACT Wazalendo kwa kauli moja imeamua kushiriki uchaguzi si kuisusia CCM ndio maana wamekuja na kauli mbiu ya Oktoba linda kura wakiwa na maana ya kuwaamsha Watanzania kupiga kura ili kuipa thamani.

Katika maelezo ya Zitto amesema walianza ziara katika Mkoa wa Tabora, wakaenda Katavi, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Lindi, Mtwara na Pwani ambapo wamekutana na changamoto mbalimbali zikiwemo umasikini, tembo kuvamia makazi, ushuru wa mazao, kilio cha ajira, migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji.

Zitto amesema changamoto hizo zinazowakabili Watanzania haziwezi kutatuliwa kwa kuiacha CCM pekee yake madarakani au bungeni badala yake vyama vinapaswa kushiriki uchaguzi si kukimbia chama tawala.

“Tusiwaachie CCM wawe pekee yao bungeni au kutawala Barazala Wawakilishi Zanzibar, haya mwaka 2019 CCM walichukua vijiji, vitongoji na mitaa yote na mwaka 2020 walichukua karibu majimbo niwaulize changamoto zenu zimeisha? Zitto akajibiwa hapana na wananchi.

“Haya barabara ya Utete -Nyamwage imejengwa na kukamilika? Nawauliza watu wa Rufiji akajibu hapana…niambieni au wapinzani tuliwachelewesha, maana walikuwa pekee yao kuanzia madiwani hadi wabunge,” amesema Zitto.


Zitto amesema miaka mitano mingine haipaswi kuachwa peke yao bali upinzani ushiriki uchaguzi ili kukabiliana na CCM katika sanduku la kura Oktoba.

Naibu Katibu Mkuu ACT Wazalendo (Bara), Esther Thomas amewaambia wananchi Rufiji kuwa ni mwaka huu ni wakati mwafaka wa kufanya mabadiliko ili kuchagua viongozi watakaowateteea na kuwaleta maendeleo sio wale wanaojitapa.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo, Kiza Mayeye amesema katika maeneo mbalimbali waliopita na viongozi wenzake wamebaini bado Watanzania wanaishi katika mazingira magumu kutokana umasikini.

Mayeye ambaye amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu, amewataka kina mama wa Rufiji kusimama imara ili kumpeleka bungeni mtiania wa jimbo hilo, Kuluthum Mchuchuli ambaye aliwahia kuwa mbunge wa viti maalumu.

“Simameni imara mpelekeni Mchuchuli mwezenu akasimame imara wa kusimamia changamoto zinazowakabili ikiwemo huduma afya zisizoridhisha,” amesema Mayeye.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Janeth Rithe amesema pamoja ja mambo mengine ziara hiyo ina lengo la kuzungumza na Watanzania ili kufanya mabadiliko katika uchaguzi mkuu wa Oktoba baadaye.

Kwa upande wake, Mchuchuli amesema licha ya Rufiji kuwa na neema ya kupata miradi mbalimbali lakini hakuna ambacho wananchi wananufaika, kutokana na maendeleo kusuasua.

Related Posts