Dar es Salaam. Serikali imewakaribisha wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza katika uongezaji thamani wa mazao yanayopatikana nchini kwani malighafi zinapatikana kwa wingi, hivyo gharama za uzalishaji zitakuwa nafuu kwao.
Hayo yamebainishwa leo Julai 15, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa jukwaa la biashara la Tanzania – India lenye lengo la kuwafungulia fursa zinazopatikana Tanzania wawekezaji kutoka India waliokuja nchini kujifunza.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema Tanzania na India zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu kwenye maeneo ya kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni.
Amesema Tanzania imekuwa ikiuza India malighafi badala ya bidhaa zilizoongezwa thamani hasa kwenye sekta ya kilimo. Amesema Tanzania imekuwa ikiuza India korosho ghafi, mbaazi na mazao mengine.
“Moja ya maeneo tunayoyaangalia ni kuona namna gani tunawavutia wenzetu wa India kuja kuwekeza Tanzania kwenye uongezaji thamani kwenye mazao ya kilimo. Pia, Tanzania tumekuwa waingizaji wa bidhaa mbalimbali kutoka India hasa dawa,” amesema.
Kigahe amesema zaidi ya asilimia 85 ya dawa zinaagizwa nje ya nchi na sehemu kubwa ya dawa hizo na vifaa tiba, zinatoka India, hivyo wamekutana kujadiliana nao namna ya kuwekeza kwenye viwanda vya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba hapa nchini.
Amesema malighafi nyingi za kuzalisha dawa na vifaa tiba zinapatikana hapa nchini kama vile pamba na nyinginezo. Amesema hiyo ni fursa kwa wawekezaji wa India na pia Tanzania itanufaika kwa kupata dawa hapahapa.
“Eneo jingine tunataka waje kuwekeza katika sekta ya usafirishaji. Tunataka waje kuwekeza katika uzalishaji wa vipuri vya treni. Wenzetu Wahindi walishaendelea kwenye eneo hilo, hivyo ni muhimu wakaja kuwekeza kwenye viwanda vya vifaa hivyo,” amesema.
Amesema kwenye eneo la Tehama, India wamepiga hatua, hivyo wanawashawishi waje kuwekeza ili kutumia fursa hiyo kufanya biashara na Watanzania. Amesema wizara yake inaratibu mazungumzo hayo ili wawekezaji hao waje.
Naibu Waziri huyo amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kwenye maeneo kama vile madini, kilimo, mawasiliano, viwanda. Hivyo, wanaendelea kuvutia uwekezaji kwani mazingira ya uwekezaji sasa yameboreshwa.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini India, Hamisa Mbega amesema moja ya majukumu waliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini Tanzania.
“Huu ujumbe wa wafanyabiashara tuliokuja nao umejikita zaidi katika kuwekeza katika maeneo makuu mawili kwa kuanzia; eneo la uzalishaji wa dawa na vifaa tiba na eneo la kilimo hasa uongezaji thamani wa mazao yetu,” amesema Balozi Mbega.
Amesema ujio wawekezaji hao ni katika jitihada za kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba katika ukanda huu. Amesema kuna fursa kubwa kwa Wahindi na kwa Watanzania endapo viwanda vya dawa vitaanzishwa hapa nchini.
Balozi Mbega ameongeza kuwa India imepiga hatua kwenye sekta ya kilimo na kupitia ushirikiano uliopo, Tanzania inaweza kuboresha kilimo chake na kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi kwa kuongeza thamani mazao yao.
Mkurugenzi wa Uwezeshaji kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), George Mukono amesema taasisi hiyo inakwenda kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050, hivyo ilikutekeleza hilo, wanatakiwa kuwawezesha Watanzania kuhodhi uchumi wao.
“Kupitia taasisi hii ya Tiseza, tunawahamasisha wawekezaji wazawa waweze kuungana na wawekezaji kutoka nje ili kuongeza ufanisi zaidi katika uzalishaji ili kufikia uchumi wa juu kama dira ilivyoelekeza,” amesema.