Hizi hapa fani zinazopendwa na wengi vyuo vikuu

Dar es Salaam. Wakati dirisha la kuomba udahili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu likifunguliwa rasmi, takwimu zinaonyesha fani nne ndiyo zinazopendwa zaidi na wanafunzi.

Kwa mujibu wa takwimu mpya za Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) zilizotolewa Mei 2025, takribani asilimia 70 ya wanafunzi waliojiunga na vyuo vikuu mwaka 2024/2025  walichagua masomo ya biashara, elimu, sayansi ya jamii na fani za  udaktari na afya.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa mbali na mwaka huo, fani hizo pia ndizo zilizoongoza kusomwa na wanafunzi wengi kwa miaka minne mfululizo kati ya mwaka 2021/20 hadi mwaka 2024, hatua ambayo pengine inaashiria kuwa masomo hayo ndiyo yanayoongoza kwenye soko la ajira.

Kati ya wanafunzi 151,882 waliodahiliwa mwaka wa masomo wa 2024/2025, 106,249 walichagua masomo hayo,  huku wadau wakisema idadi hiyo inachangiwa na urahisi wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi.

Aidha, fani kama ya biashara inatajwa kuwawezesha wanafunzi kujiajiri, huku wanaosoma fani za afya na ualimu wakiwa na matumaini ya kupata ajira za moja kwa moja ama serikalini au katika sekta binafsi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, masomo ya biashara ndio kinara kwa kusomwa na  wanafunzi wengi wanaojiunga vyuo. Kuna ukuaji wa asilimia 42.35 ndani ya miaka hiyo minne, huku wanafunzi 51,906 wakitajwa kuchukua masomo hayo kwa mwaka 2024/25

 Masomo ya sayansi ya jamii yamekua kwa asilimia 21.4, elimu (18.14%) na fani ya udaktari na dawa (10.71%).

Kwa idadi ya udahili wa  wanafunzi  kwa masomo mengine mwaka 2024/ 25 ilikuwa kama ifuatavyo: elimu (25,675 ), sayansi ya jamii   (18,126 ) na fani za udaktari na afya (10,542)

Hata hivyo, tofauti na fani nyingine, kati ya mwaka 2023/2024 na 2024/2025,  wanafunzi waliodahiliwa kusoma fani ya ualimu walishuka kwa asilimia 16.42.

Akizungumza maana ya takwimu hizo na sababu ya wanafunzi wengi kuchagua fani hizo, mdau wa elimu, Ochola Wayoga amesema uwepo wa uhakika wa  mikopo, wanafunzi wengi kusoma masomo ya sanaa  wakiwa ngazi ya chini na ajira ndiyo sababu ya wengi kuangukia katika fani za ualimu, biashara na sayansi ya jamii.

“Ualimu zamani mtu alikuwa na uhakika wa kupata mkopo na ajira ndiyo maana wengi walikuwa wakichagua kuusoma. Biashara na sayansi ya jamii ni msingi ambao watu wako nao tangu mwanzo, wengi hawakuwa wamesoma sayansi ndiyo maana wameangukia huko pia wanaangalia uwezekano wa kuajirika,” amesema.

Hata hivyo, akizungumzia kupungua kwa idadi ya wanaokwenda ualimu,  amesema wengi wanaamua kutafuta fursa sehemu nyingine baada ya walimu wengi kuwa mtaani bila ajira.

“Lakini kupungua huku kunaweza kuwa na faida kwani kunaweza kutoa mwanya kwa wale waliomaliza kupata fursa ya ajira,” amesema Wayoga.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya ubunifu katika elimu Tanzania (EIT), Benjamin Nkonya amesema fani hizo zinakimbiliwa na watu kutokana na urahisi wa kupata mkopo.

Lakini anasema changamoto inakuja pale wanapohitimu,  kwani baadhi huamua kutumia fedha wanazozipata kwenye mikopo kama mitaji kutokana na kutokuwapo kwa ajira baada ya kuhitimu masomo.

“Kuna haja ya kuangalia mfumo wa utoaji mikopo hii badala ya kuangalia tu mtihani wa kidato cha sita, kuna ofisi inayohusika na masuala ya kazi waangalie ni taaluma gani inahitajika katika soko la ajira kila mwaka na hao ndiyo wapewe mikopo,” amesema.

Amesema wale ambao taaluma zao hazihitajiki zaidi sokoni wajigharamie wenyewe ili nchi iweze kutengeneza wataalamu wa kutosha wanaohitajika kuziba nafasi zilizo wazi,” amesema Nkonya.

Dirisha la udahili Kuhusu mchakato wa wanafunzi kuanza kuomba nafasi vyuoni, TCU imewataka waombaji wa shahada ya kwanza kusoma miongozo na programu za vyuo husika,  kabla ya kuomba ili kuondoa uwezekano wa kuchagua kozi ambazo hazipo.

“Leo tunafungua awamu ya kwanza ya dirisha la udahili katika mwaka mpya wa masomo itakayodumu kwa siku 26, msisitizo kwa waombaji ni kusoma miongozo na kupata taarifa rasmi kutoka vyuo husika sio kusikia habari za mtaani,’’ amesema Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa.

Ameongeza: “Kama unataka kusoma programu fulani hakikisha kwamba inapatikana kwenye hicho chuo unachotaka kusoma. Kwa maboresho haya ambayo yamefanyika upo uwezekano kuna programu zimefutwa au kubadilishwa hivyo ni lazima uwe makini.’’

Related Posts