Dar es Salaam. Mtoto mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka mitatu hadi minne amefariki dunia kwa ajali ya moto uliotokea kwenye chumba kimojawapo katika ghorofa eneo la Magomeni Kota, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi Jacob Chacha amethibitisha kutokea tukio hilo saa 11:17 jioni ya leo Julai 15, 2025.
Katika uchunguzi wa awali walioufanya, Kamanda Chacha amesema chanzo cha ajali hiyo ni mtoto huyo aliyefariki dunia aliyekuwa ndani ya chumba ulipotokea moto kuchezea njiti za kiberiti na wakati anafanya hivyo hakukuwa na uangalizi wa mtu yeyote.
“Baada ya kufika eneo la tukio tulipambana kuudhibiti moto, ingawa chumba kimoja kiliungua, lakini jengo hilo lenye ghorofa saba na lina Kaya 128 halikupata madhara zaidi,” amesema.
Ameongeza kuwa “Wakati tunapambana kuudhibiti moto kuna mtoto mmoja wa kiume anayekadiriwa kuwa na miaka mitatu hadi minne alifariki dunia kutokana na moshi na moto,” amesema.
Amesema mtoto huyo kwenye chumba hicho alikuwa peke yake, japo aliweza kutolewa mahali alipokuwepo na kupelekwa hospitali lakini madaktari walithibitisha amefariki dunia.
“Ni muhimu wazazi au walezi kuwa makini na watoto wao muda wote, kwa sababu anatakiwa kuchungwa muda wote ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema.
Mwenyekiti wa Magomeni Kota, Gorge Abel amesema mtoto huyo alikuwa chumbani peke yake wakati dada yake alikuwa ametoka nje na wazazi wake walikuwa kazini.
“Ilikuwa taharuki Kikosi cha Zimamoto hawakufika kwa wakati, na walipokuja ilichukua muda kufikisha maji kwenye ghorofa ya saba na hapa tuna changamoto ya maji,” amesema.
Mwenyekiti huyo ameshukuru kwa jitihada zilizofanyika na jeshi hilo hadi kufanikiwa kudhibiti mapema bila kusambaa kwenye vyumba vingine.