Wapenzi wa safu hii, napenda kuwasalimia na kuwakaribisha kwenye makala hii ya ushauri. Mimi ni mwandishi wa habari wa kujitegemea na kwa muda mrefu nimekuwa pia mdau mkubwa wa maonesho mbalimbali hapa nchini.
Kwa wengi, Maonyesho ya Sabasaba au Dar es Salaam International Trade Fair (DITF) yanachukuliwa kama maonesho makubwa zaidi nchini Tanzania. Sababu kubwa ni kwamba ni maonesho ya kimataifa yanayofanyika kwa pamoja katika eneo moja lililoandaliwa vizuri viwanja vya Mwalimu Nyerere Sabasaba.
Hata hivyo, tukichambua kwa uhalisia, Tanzania ni nchi inayotegemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 65 ya ajira na sehemu kubwa ya Pato la Taifa. Hivyo, kwa vigezo vya maana kwa wananchi walio wengi, Maonyesho ya Nanenane ndiyo yanapaswa kuwa makubwa na yenye umuhimu zaidi kuliko yote nchini. Changamoto yake kubwa ni kwamba yamegawanyika kwa kanda mbalimbali, jambo linalopunguza mvuto na uwekezaji wa pamoja kama ulioonekana kwenye Saba Saba.
Makala hii inalenga kutoa ushauri wa wazi: tufanye maboresho makubwa ya Maonesho ya Nanenane kwa kujifunza na kuiga yaliyofanywa kwenye Sabasaba. Tuweke nguvu sawa, miundombinu bora na huduma za kisasa. Kama taifa moja, hatupaswi kuwa na maonesho mawili makubwa – Sabasaba na Nanenane – kisha moja lipambwe na miundo bora ya kisasa yenye barabara za lami na majengo yenye viyoyozi, wakati jingine likibaki na mabanda ya mahema na barabara za vumbi.
Pongezi zangu kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kazi nzuri ya kuboresha Sabasaba tayari niliitoa kwenye makala iliyopita.
Leo nazidi kutoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake, kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kuhimiza juhudi za kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania, hususan za kilimo, kwenye masoko ya nje ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Waziri Mkuu Majaliwa, akimwakilisha Rais Samia katika kufunga Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam Julai 13, 2025, aliagiza TanTrade kufanya tafiti na uchambuzi wa masoko ili kutoa taarifa sahihi kwa wafanyabiashara. Alisema:
“Masoko yamekuwa ya ushindani sana siku hizi… tunapofanya uchambuzi wa masoko yetu, tuangalie Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)… TanTrade fanyeni tafiti za uhakika na uchambuzi wa kina.”
Pia, alihimiza wazalishaji nchini kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa zenye mahitaji makubwa ndani na nje ya nchi, akisisitiza umuhimu wa ubora ili bidhaa ziweze kushindana kimataifa. Aliwakumbusha pia umuhimu wa kutumia alama ya taifa kwenye bidhaa, akisema: “Hakikisha pale chini umeandika Made in Tanzania, hiyo ndiyo nembo yetu ya Taifa.”
Aidha, Waziri Mkuu aliagiza taasisi zote za biashara na uwekezaji – Tanzania Bara na Zanzibar – kuondoa urasimu unaokwamisha biashara na badala yake kuwezesha biashara na uwekezaji. Aliahidi pia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji katika maeneo ya kimkakati ili kuchangia pato la taifa na kunufaisha wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo alieleza kuwa katika siku 16 za maonesho, watu zaidi ya milioni 2.4 walishiriki kwenye shughuli mbalimbali za Sabasaba. Alisisitiza umuhimu wa kutumia alama ya Made in Tanzania kama sehemu ya kujiuza kimataifa na kujenga fahari ya taifa. Ni vizuri kufahamu kwamba ingawa TanTrade ipo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, maonesho ya Nanenane yanasimamiwa na Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Ikiwa kweli tunataka Nanenane nayo iwe ya kimataifa na yenye hadhi sawa na Sabasaba, basi TanTrade iruhusiwe kuandaa maonesho hayo kwa ushirikiano na wizara husika. Hii itahakikisha kuwa maboresho ya Sabasaba, barabara za lami, majengo ya kisasa, viyoyozi na huduma bora yanatekelezwa pia kwenye Nanenane kote nchini.
Tanzania ni nchi moja. Haipendezi kuona wageni wa kimataifa wakienda Sabasaba kwenye viwanja vya kisasa vya viyoyozi, kisha wakienda Nanenane kwenye vibanda vya mahema na barabara za vumbi. Hii ni fursa ya kubadilika na kufanya Nanenane kuwa chombo cha kweli cha kuendeleza kilimo na kukuza biashara za mazao yetu kitaifa na kimataifa.