Josiah awapa saluti Lazaro, Ahmad Ally

KOCHA wa Tanzania Prisons, Aman Josiah amewataja makocha waliyofanya vizuri msimu ulioisha ambao ni Ahmad Ally wa JKT Tanzania na wa Coastal Union, Joseph Lazaro, akiwaweka kando wa timu zilizomaliza Top 4 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Alitoa sababu ya kwa nini Ally ambaye timu ilimaliza nafasi ya sita ikiwa na pointi 36 na Lazaro kikosi chake kikimaliza nafasi ya nane kwa alama 35 kwamba mbinu zao ziliwabeba tofauti na makocha wa Top 4 ambao wamezungukwa na vitu vingi, vilivyowarahisishia kazi.

“Naheshimu sana walichokifanya makocha wa Simba, Yanga, Azam FC na Singida Black Stars, lakini hizo timu zilizungukwa na wachezaji wa viwango vya juu na hali zao kiuchumi ni nzuri, ukilinganisha na timu nyingine zilizoshika nafasi ya chini yao,” alisema Josiah na kuongeza;

“Ni kweli Top 4 zinazoongoza kwa takwimu za wafungaji kama kinara wa mabao 16 Jean Ahoua (Simba), Clement Mzize mabao 14 (Yanga), Jonathan Sowah 13 (SBS) na Gibril Sillah (Azam) hao ndiyo wafungaji wao namba moja na viwango vyao vipo juu, lakini anayeongoza JKT Tz ni Edward Songo ana mabao sita, Coastal ni Maabad Maulid mabao matano lakini wanajipambania zaidi kufanikisha mabao hayo.”

“Mbali na hao wapo wachezaji wasiotajwa kama Haruni Chanongo wa Prisons ana mabao manne, kuna Jacob Masawe wa Namungo hao jamaa ni wazuri kwa mbinu,” alisema.