Hatimiliki za ardhi 1,176 zatolewa Sabasaba

Dar es Salaam. Jumla ya hatimiliki 1,176 zimetolewa katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yaliyofikia tamati Julai 13, 2025 jijini hapa.

Hatimiliki hizo zimetolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika maonesho hayo yaliyobeba kaulimbiu ya “Fahari ya Tanzania”.

Akizungumza baada ya kufungwa kwa maonyesho hayo, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia wilaya ya Ilala na Temeke, Rehema Mwinuka amesema kati ya hati zilizotolewewa 1,040 zimetolewa kwa wamiliki wa Mkoa wa Dar es Salaam na 68 ni kwa Mkoa wa Pwani.

Rehema amesema mbali na kutoa hati hizo pia Wizara ya Ardhi katika maonesho hayo ya Sabasaba ilihudumia zaidi ya wananchi 1,616 waliofika kuhitaji huduma za sekta ya ardhi katika maeneo mbalimbali.

Afisa Utumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mwajabu Masimba (kulia) akimkabidhi Hati ya Ardhi Msanii wa Bongo Movie Richie Mtambalike wakati wa Maonesho ya Sabasaba jijini Dar Es Salaam.



“Katika maonesho ya mwaka huu wizara yetu ilijipanga kutoa huduma mbalimbali na imefanikiwa kuwahudumia zaidi ya wananchi 1,616 huku hati 1,176 zikitolewa,” amesema Rehema.

Baadhi ya wananchi waliofika Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi walionesha kuridhishwa na huduma zilizokuwa zikitolewa wakati wote wa maonesho na kusisitiza umuhimu wa Wizara ya Ardhi kuandaa huduma ya pamoja (One Stop Center) ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za sekta ya ardhi.

Walitolea mfano wa huduma ya utoaji hati miliki za ardhi pamoja na ukadiriaji kodi ya pango la ardhi kuwa, ni moja ya huduma iiliyopatikana kwa haraka jambo linaloonesha kuwa, wizara ilijipanga katika maonesho hayo.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaan Shukrani Kyando (kulia) akimkabidhi hati milki ya ardhi Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar Es Salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Dk Lazaro Mambosasa wakati wa maonesho ya kimataifa ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.



Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha, Aisha Bade ambaye ni mmoja wa waliopata hati milki ya ardhi katika maonesho hayo amesema Wizara ya Ardhi kwa sasa imebadilika kwani huko nyuma kupata hati ilichukua zaidi ya mwaka.

“Niwapongeze Wizara ya Ardhi kwa hatua mliyofikia, huko nyuma kupata hati miliki ya ardhi ni ‘issue’ lakini leo nimeipata hati yangu ndani ya muda mfupi, hongereni sana,” amesema.

Naye Muigizaji wa Bongo Movie, Richie Mtambalike ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa kutoa huduma za papo hapo hasa utoaji wa hati milki za ardhi katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba.

Msajili kutoka Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Lemuel Ngowi akizungumza na wanafunzi waliotembelea banda la chuo hicho wakati maonesho wa kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.



“Niishukuru Wizara ya Ardhi kwa kutuletea huduma hapa katika maonesho maana kwa upande wangu nimefanikiwa kupata hati milki ya arhi hapa hapa,” amesema.

Katika maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu Wizara ya Ardhi ilitoa huduma za sekta ya ardhi kwa mkoa wa Dar es salaam ikihusisha Manispaa za Kinondoni, Ubungo, Kigamboni, Ilala na Temeke, Mkoa wa Pwani pamoja na Dodoma.

Mwandishi Mkuu wa Sheria Onorius Njole (wa tatu kulia) akimsikiliza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia wilaya ya Ilala na Temeke Rehema Mwinuka (kushoto) alipotembelea banda la wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa maonesho wa kimataifa ya Baishara (Sabasaba). Kulia ni Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam Burton Ruta 



Pia ilitoa elimu kuhusiana na masula ya sekta ya milki, urasimishaji makazi holela, Mbaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya pamoja na namna ya kujiunga na Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) katika masomo kwa ngazi ya astashahada na stashahada.