Mwalimu auawa Geita kwa kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali

Geita. Mwalimu Dorosela Salvatory (45) wa Shule ya Sekondari Nyanza amekutwa amefariki dunia akidhaniwa kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha tukio hilo akisema limetokea jana Jumanne, Julai 15, 2025 ndani ya nyumba ya mwalimu huyo iliyoko Mtaa wa Uwanja, Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita.

Kutokana na tukio hilo, mtu mmoja Nickson Jonson (54), Mkazi wa Geita anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi akituhumiwa kuhusika na mauji hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, mwili wa mwalimu huyo umekutwa ukiwa ndani ya nyumba yake ukiwa umekatwakatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.

Jongo amesema polisi inaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo na taarifa kamili itatolewa mara baada ya uchunguzi kukamilika.

Aidha Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea ili waliohusika waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mmoja wa walimu wa Shule ya Nyanza ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema mwalimu huyo hakufika kazini Julai 15 na aliyegundua mauaji hayo ni mtoto wa marehemu aliyetoka shule na kukuta mwili ukiwa umejaa damu ukiwa chini sakafuni.

“Mtoto wake anayesoma darasa la tano amesema asubuhi mama yake alimpeleka kupanda gari la shule hakujua kilichoendelea hadi aliporudi kuingia ndani akakuta mwili chini umekatwakatwa ndio akapiga kelelele za kuomba msaada,” amesema Mwalimu huyo.