Dar es Salaam. Wakati matukio ya watu kujiua yakiendelea kutokea kwa kile kinachoelezwa kuwa ni msongo wa mawazo, jamii imetakiwa kutambua kuwa afya ya akili ni tatizo kubwa na watu wasaidiwe kabla ya kufanya maamuzi yasiyo sahihi kama kujiua.
Hivi karibuni yameripotiwa matukio mawili ya vijana kujiua mmoja akiwa mfanyabiashara na mwingine daktari wa watoto ambayo yote yametokea mkoani Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi Ronald Malisa (35) ambaye alikuwa mfanyabiashara wa Moshi na Dodoma anadaiwa kujiua kwa kujinyonga katika choo cha nyumba yake.
Ilielezwa kuwa tukio hili lilitokea Julai 10 chanzo ni msongo wa mawazo na mara kadhaa alishajaribu kutaka kujiua kwa kunywa sumu ila alikuwa akiokolewa na wanafamilia.
Siku hiyo hiyo lilitokea tukio lingine ambapo Magreth Swai ambaye alikuwa daktari naye alijinyonga.
Kufutia mfululizo wa matukio hayo Mwananchi imezungumza na Carol Ndosi ambaye ni miongoni mwa watu waliowahi kupata msongo wa mawazo na aliyejaribu kujiua mara kadhaa.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Julai 16, 2025 kwa njia ya simu Carol amesema kinachowasumbua Watanzania wengi ni kutokubali kwamba changamoto ya afya ya akili ni tatizo kubwa na ukiwa nalo unapaswa kukubaliana na hali hiyo kisha utafute msaada.
Amesema ni muhimu kwa wanajamii kufahamu dalili na pale mtu anapojihisi kwamba ana changamoto hivyo awe tayari kukubaliana nayo na kutafuta msaada hasa kuzungumza na wataalamu wa afya ya akili na ushauri.
“Tunapaswa kujikumbusha kwamba afya ya akili ni tatizo kubwa hivyo ni vyema tukajifunza kukabiliana nalo baada ya hapo ndipo utafute msaada.Tusibeze hawa waliojuiua au wanaojaribu kujiua hili tatizo lipo na ni kubwa.
“Kinachotokea ni kukabiliana na ile sauti unayoisikia ndani yako. Nikiwa miongoni mwa watu ambao walikutana na mawazo ya kutaka kujaribu kujiua naona kuna umuhimu mkubwa wa kuwaona wataalamu ambao unaweza kuzungumza nao.”
Mwanasaikolojia Mallewo Charles amesema kuna umuhimu mkubwa wa watu kuwa tayari kuwasikiliza wengine wanapokuwa na changamoto kwa sababu kusikilizwa ni mojawapo ya tina kwa mtu mwenye tatizo la afya ya akili.
“Hakuna kitu cha gharama kama kumsikiliza mtu na kumuelewa ni tiba, hautapungukiwa chochote ukitenga muda wako kumsikiliza mwenzio mwenye matatizo na ukaonesha kumuelewa na kuvaa viatu vyake.
“Ukimsikia mtu anazungumza maneno yanayoashiria kukata tamaa, kupoteza thamani yake mpe matumaini kama huwezi mshauri aende kwa watalaamu usifanye utani wala kumpa maneno ya kejeli,”
Akizungumzia hilo Mkurugenzi wa asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Rustika Tembele amesema Tanzania inaweza kukabiliana na matukio ya watu kujiua endapo jamii itarudi kwenye msingi wa maisha ya upendo na ujamaa.
Tembele amesema matukio hayo yanaendelea kutokea wakati yangeweza kuzuilika kwa kuwa mtu anayefikia kujia hafikii uamuzi huo bila kuwepo sababu.
“Mfumo wa maisha umebadilika, watu hawajali shida za wengine ndio kwanza wanafurahia kumbe hujui yule unayemfurahia matatizo yake ungekuwa naye karibu kumfariji huenda asingefikia uamuzi wa kujiua.
Sasa hivi hata ukiona mtoto wa jirani yako ana mienendo isiyofaa au hata ishara za kujidhuru unashindwa kumhoji au kuzungumza naye kwa kuwa anaweza kukutukana, hii ni mbaya tunaishia kuongea baada ya kifo kuwa alikuwa na dalili za kujiua,” amesema Rustika.
Amesema ni muhimu kwa wanajamii kuwapa matumaini watu walielemewa na mizigo kwenye mioyo ili kuwanusuru na matatizo ya afya ya akili ambayo yanaweza kumsukuma mtu kujitoa uhai.
“Tusiwaite majina ya kuwakatisha tamaa mfano dishi limeyumba, mtambo, chizi, chupa imeamka na chai, golikipa katola golini, hii yote ni misemo ya unyanyapaa haifai inaweza kumfanya mtu kukata tamaa na kuamua kujiua,” amesema.
Dalili za mtu anayetaka kujitoa uhai
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeainisha dalili kadhaa ambazo akionekana nazo mtu kuna uwezekano akafirikia kujitoa uhai.
Dalili hizo ni pamoja na mtu kulala sana na kupenda kujitenga na wengine na mara nyingi kujifanyia mambo kivyake.
Nyingine ni kupoteza matumaini ya kuishi, kujiona hana msaada, thamani na kujichukulia kuwa mzigo kwa wengine au kuzungumzia kukosa umuhimu wa kuishi.
Mtoa huduma za ushauri nasaha Sixtha Komba ambaye alithibitisha kuwepo watu wengi mitaani wenye dalili ambazo zimeanishwa na WHO hivyo zinahitajika jitihada kuwanusuru.
Amesema katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo hufanya kwa ngazi ya mtaa amebaini kuwa watu wengi wanapitia changamoto zinazowasababishia misongo ya mawazo.
“Tatizo la kujiua halizungumziwi ila lipo na jamii inachangia kwa kiasi kikubwa kumfanya mtu kufikia hatua hii. Hakuna upendo, watu wako busy na maisha kuliko kujali hali ya mwingine.
Tunakutana na watoto wanasema wazazi wao hawana muda wa kukaa nao, baba na mama wanatoka asubuhi na kurudi usiku wanakuta mtoto ameshalala, hali ile inamfanya mtoto kujiona hana thamani anaanza kuweka vitu moyoni,”alisema.
Sixtha amesema kujaza vitu moyoni kunaweza kumsababisha mtoto yule kuchukua aumuzi wa kujiua au kujidhuru kwa namna yoyote kwa anahisi hana thamani.
Kwa upande wake Victoria Nakajumo ambaye pia ni mnasihi amesema ipo haja ya watu kutafuta watu wanaowaamini kuzungumza nao kuhusu yanayowakabili kuliko kuyaweka moyoni.
“Unapoweka mambo moyoni unasababisha sumu na kujibebesha mzigo unaoweza kukufanya uchukuea uamuzi mbaya, tafuta, unayemuamini zungumza naye na wewe unayeaminiwa basi kuwa tayari kumpa nafasi mwenzio akuelezee, umshauri na ubaki nayo uliyoambiwa,” amesema Victoria.